KISPOTI:
MIKONO YA NDUDA INALALAMIKA.
Na Prince Hoza
MASHABIKI na wapenzi wa Simba SC kuna wakati hawaeleweki kabisa, wao wanapenda starehe tu, shida ama taabu kwao si rafiki kabisa na hawataki kusikia kitu kama hicho, ukiwa na shida zako hawana habari na wewe wao wanachapa mwendo, hao ndio mashabiki wa Simba ambao wanacheka kwa dharau.
Wanacheka kwa dharau kwa sababu timu yao kwa sasa ipo katika ubora wa hali ya juu, kikosi cha Simba kinaendeleza kutoa dozi kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba ilianza ligi kwa kishindo baada ya kuichapa Ruvu Shooting ya Mlandizi Pwani mabao 7-0 kabla haijalazimishwa sare isiyo ya mabao 0-0 na Azam FC ikiwa ni mechi yake ya kwanza kucheza ugenini, mechi hiyo ilipigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Dar es Salaam.
Lakini mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba iliivulumishia Mwadui FC ya Shinyanga mabao 3-0 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, ushindi huo umeiwezesha Simba kufikisha pointi 7 na ikikamata nafasi ya pili nyuma ya vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar wenye pointi 9, baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza.
Lakini Simba ndio timu yenye mabao mengi zaidi, ikifunga mabao kumi huku mchezaji wake Emmanuel Okwi raia wa Uganda akiongoza kwa ufungaji wa magoli, mpaka sasa Okwi amefunga magoli 6 na wanaomfuatia kwa vyovyote watakuwa wamefunga magoli mawili.
Hapo utaona tu jinsi mashabiki wa Mnyama wanavyocheka kwa dharau, hawama habari kwani timu yao inawapa raha, watani zao Yanga wako taabani kwani hadi sasa wamecheza mechi tatu kama ilivyo Simba lakini wameambulia pointi tano, Yanga wameambulia sare mechi mbili na wakishinda mechi moja tu.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, walianza ligi kwa kushikwa shati na Wanapaluhengo, Lipuli ya Iringa wakifungana bao 1-1 mchezo uliofanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Yanga ilisawazisha goli ikitaka kulala mbele ya vijana hao wanaonolewa na kiungo wa zamani wa Simba, Seleman Matola "Veron".
Yanga ikapata ushindi wake wa kwanza mjini Njombe baada ya kuilaza Njombe Mji FC bao 1-0 bao ambalo walilipata kwa mpira wa faulo likifungwa kistadi na Ibrahim Ajibu, mabingwa hao wakabanwa mbavu na Majimaji katika mchezo mwingine wa ligi uliofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea, Jumamosi iliyopita.
Yanga na Majimaji zilifungana bao 1-1, hivyo wanarejea Dar es Salaam na pointi nne walizozipata huko Nyanda za juu kusini, watani zao Simba wanacheka kwa dharau hasa baada ya Yanga kuboronga kiasi hicho, safu ya ushambuliaji ya Yanga hadi sasa imefunga mabao matatu tu huku yakiwa yameachwa mbali na mchezaji mmoja wa Simba, Emmanuel Okwi mwenye mabao sita peke yake.
Simba sasa wanajiandaa kuifuata Mbao FC jijini Mwanza katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, hiyo ndiyo Simba, Lakini kwa upande mwingine kuna changsmoto zake toka kwa mashabiki wake, mashabiki wake hawana simile, Timu yao ikitokea kufanya vibaya hata kwa kutoka sare lawana huanzia hapo.
Hivi karibuni ililazimishwa sare tasa na Azam FC ya 0-0 katika uwanja wa Azam Complex, mashabiki wa Simba walianza kumlakamikia kocha wao Mcameroon Joseph Omog wakidai ameshindwa kukinoa kikosi hicho, mashabiki hao walikuwa wakimtaka Jonas Mkude.
Hata kwenye mchezo wa jana dhidi ya Mwadui, mashabiki wa Simba walikuwa wakimlaumu Omog kwa kitendo chake cha kuwatoa Shiza Kichuya na Nicolaus Gyan, mashabiki hao walitaka John Bocco "Adebayor" atolewe, lakini Bocco alipofunga goli la tatu ambalo lilikuwa maridadi ambalo liliwanyamazisha mashabiki hao.
Mechi zote hizo tatu, Simba imemwanzisha langoni kipa wake Aishi Manula, na kipa mwingine Emmanuel Mseja amekuwa akianzia benchi, lakini Simba msimu huu imesajili makipa watatu akiwemo na Said Mohamed Nduda, Nduda alikuwa kipa wa kwanza wa Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro.
Kwa bahati mbaya kipa huyo ni majeruhi, Nduda aliumia mazoezini kule Zanzibar wakati Simba ilipoenda kuweka kambi kujiandaa na mchezo wake wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Nduda alisajiliwa na Simba baada ya kuibuka kipa bora wa michuano ya Cosafa Castle Cup iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Umuhimu wa Nduda katika kikosi cha Simba kwa sasa hauonekani kabisa, hata viongozi wa timu hiyo kwa sasa wanasikilizia tu, awali kipa huyo ilikuwa asafirishwe haraka kwenda India kufanyiwa matibabu, lakini safari hiyo haikuwemo na kilichobakia kwao ni kutoa maelezo kwamba watampeleka India.
Mashabiki wa Simba hawana habari naye kwa sababu kipa Aishi Manula hajaruhusu hata bao moja langoni kwake, unamuwazaje kipa mwingine kwa mfano, Said Mohamed Nduda kwa vyovyote anasubiri safari, mikono yake inalalamika, na inalalamika kwa sababu achezi.
Lakini mashabiki wa Simba wataupigia kelele uongozi wao kuhusu kuchelewesha matibabu ya kipa huyo iwapo tu Aishi Manula atafungwa magoli ya kizembe, wako wapi Vincent Angban na Daniel Agyei, ukipata majibu walipo basi Simba isizuge kwa Said Mohamed na afanyiwe wepesi ili atibiwe haraka na arejee kazini.
Said Mohamed ajira yake mpira, kucheza kwake ndio kunaboresha kiwango chake, anavyozidi kukaa nje ndipo umahiri wake utakapoanza kushuka na mwishowe tutamuona kipa huyo akiangukia vitimu vya madaraja ya chini, Afya yake ni muhimu sana kwa sasa kwani nina uhakika hajaenda kutibiwa