Na Prince Hoza. Dar es Salaam
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kwenye tasnia ya filamu Duniani, tofauti na miaka iliyopita ambapo kulikuwa na wasanii wachache kwenye fani hiyo.
Lakini sasa kila kona kumetapakaa vikundi vya sanaa huku kampuni za kutengeneza filamu zikizidi kuongezeka, vijana wa kike na kiume nao wanajikita kwa wingi kwenye tasnia hiyo, tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilikuwa vigumu kuwaona vijana wakiigiza.
Miaka hiyo wazee pekee ndio waliotawala kama mzee Jangala, mzee Jongo (Marehemu), Bi Hambiliki (Naye marehemu), mzee Kagunga, mzee Janja, Bi Hindu, mzee Kipara, mzee Mahoka, mzee Pwagu, mzee Panda, mzee Majuto, mzee Small na wengineo waliweza kushiriki maigizo.
King Majuto ama mzee Majuto na mzee Small wao ndio walifungua milango kwa kufanikiwa kutengeneza filamu ambazo zilisisimua wengi na kuanza kuwavutia vijana ambao nao walianza kujiingiza kwenye tasnia hiyo, marehemu Steven Kanumba, Elizabeth Michael "Lulu", Aunt Ezekiel, Irene Uwoya, Wema Sepetu na wengineo nao waliweza kuwavuta vijana zaidi na sanaa kuzidi kutanuka.
KIKUNDI CHA NEW HOPE AMBACHO SOPHIA ANAKITUMIKIA.
.......
Mwanadada Sophia Abdul Ramadhan Kinyogoli maarufu Kibena ni miongoni mwa wasanii waliojikita kwenye filamu, Sophia yeye aliingia kwenye tasnia hiyo mwaka 2015 akiwa anasoma Kibaha, na anasema aliipenda sana sanaa hiyo mpaka akaamua kuacha shule.
Sophia anasema aliacha shule akiwa kidato cha pili na akaamua kuondoka Kibaha na kuja jijini Dar es Salaam ambapo amepokewa na baba yake mdogo pamoja na mama yake mdogo ambao anaishi nao kwa sasa maeneo ya Kawe.
Aliamua kuendelea na sanaa ambapo anamtaja kaka mmoja anayejulikana kwa jina la Gebo ndiye aliyemtafutia kikundi cha sanaa na akaungana nacho, Sophia anasema alikutana na Gebo kwenye mtandao wa facebook ambapo waliunganishiana dili humo humo.
Anasema kundi lake la kwanza lilikuwa linaitwa Chamazi Arts lililopo Mbagala Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, lakini aliishia kufanya mazoezi mpaka mwaka 2016 alipotafutiwa kikundi kingine, anasema hakuwahi kukutana na kamera zaidi ya kufanya mazoezi matupu.
Anadai kundi lake hilo ka kwanza kulitokea malumbano na wenzake hivyo akaamua kuachana nalo, anasema wakati siku zilivyozidi kusogea mbele na yeye akawa anazidi kuimarika na akawa mmoja kati ya wasanii mahiri kwenye sanaa hiyo.
SOPHIA (WA PILI KUTOKA KUSHOTO) AKIWA NA WASANII WENZAKE.
Anasema akiwa ametulia nyumbani alipigiwa simu na mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Komba ambaye anaishi Buguruni Dar es Salaam, ambapo alimjulisha kuwa anahitajika maeneo ya Mwananyamala akajiunge na wasanii wenzake waliokuwa chini ya staa Big Matovolwa ili warekodi tamthilia.
Anakiri kuwa hakuamini moyoni mwake kama kweli anahitajika kurekodi kwani hakuwahi kurekodi hata mara moja, lakini aliweza kushiriki vema kwenye tamthilia hiyo kwani wenzake walimsifia sana na kumtia moyo.
Baada ya kushiriki tamthilia hiyo akapata nafasi nyingine ya kushiriki tamthilia nyingine, safari hii akiitwa na kijana mwingine aitwaye Shafih ambaye alimpeleka katika kikundi cha New Hope kilichopo Tandale Dar es Salaam, anasema alifanyiwa usaili na akakubalika.
Sophia analitaja kundi hilo kuwa ndio limefungua njia yake ya kuelekea kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuwafikia mastaa kama Wema Sepetu ambao alikuwa akiwaona tu kupitia televisheni, akiwa na New Hope, Sophia anashiriki katika tamthilia yao ya Msitu wa Ndendemba ambayo inarushwa katika kituo cha runinga cha SIBUKA, Sophia anasema yeye alizaliwa miaka 20 iliyopita mjini Kibaha mkoani Pwani.
Anasema yeye ni mwenyeji wa Mlandizi mkoani Pwani na amekuwa akivutiwa zaidi na Wema Sepetu na Gabo na siku moja alitamani kufanya nao kazi angalau mara moja, Sophia anasema katika maisha yake amewahi kukutana na misukosuko ikiwemo ya kutoa mimba aliyopachikwa akiwa na miaka 16.
Ameongeza kuwa hata mama yake mzazi hataki kusikia yeye akijihusisha na sanaa na ndio maana aliamua kuondoka Kibaha na kuja Dar es Salaam ili kumuogopa mama yake huyo ambaye alikuwa akimkataza, lakini anasema tangia mama yake alipomuona kwenye televisheni mwenyewe akamruhusu kuendelea na sanaa akiamini siku moja atakuja kunufaika nayo
SOPHIA ABDUL MAARUFU KIBENA KATIKA POZI LA NGUVU