Joseph Kimwaga ndio basi tena
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Nadhani mnamkumbuka vema Joseph Kimwaga yule kiungo mshambuliaji wa Azam FC aliyewahi pia kusajiliwa na Simba, Kimwaga aliibuliwa kutoka Azam Academy ambapo alipangwa kwenye mchezo dhidi ya Yanga na kufunga bao la ushindi.
Katika mchezo huo Azam iliifunga mabao 3-2 mchezo wa Ligi Kuu Bara, kwa taarifa yako Kimwaga aliingia dakika za lala salama lakini alifumua bonge la shuti mpira ukaingia nyavuni na kuwalaza Yanga mchana kweupee, kuanzia hapo jina lake lilianza kujulikana.
Akaanza kupata sifa hadi akaitwa timu ya taifa, Taifa Stars, lakini aliumia na kupoteza namba kwenye kikosi cha Azam, akapotea taratibu kisha kutemwa kwenye kikosi hicho, lakini Simba wakamchukua bhana, akatua na kuanza kurudisha heshima yake iliyopotea.
Akiwa na Simba pia akapotea baada ya kuumia, Simba nao wakamtema, kijana huyo akapotea tena na hakuna aliyejua taarifa zake, ndipo alipoibuka tena baada ya Azam kumrejesha kikosini, lakini dogo kaumia tena mazoezini huko Mtwara wakati wakiwa katika maandalizi ya kuivaa Ndanda FC mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Azam walimrejesha Dar es Salaam haraka kwa kutumia usafiri wa ndege, huyo ndio Joseph Kimwaga ambaye inasemekana ndio basi tena kucheza soka kwani amekuwa akiumia mara kwa mara