Stars na Amavubi ni kusuka au kunyoa
Na David Pasko. Rwanda
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jioni ya leo inatelemka katika dimba la Nyamirambo Stadium mjini Kigali, Rwanda kurudiana na wenyeji Timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi.
Mchezo huo wa marudiano kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za nyumbani, maarufu Chan, timu hizo zilikutana Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Goli la ugenini linaonekana kuipa nguvu Rwanda, kupitia kwa kocha wake mkuu, Antoine Hey kwamba wanamaliza tu kwani ushindi walishaupata Mwanza, lakini kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema vijana wake hawatamwangusha na wataipeperusha vema bendera ya Tanzania.
Nahodha wa Tanzania, Himid Mao ambaye ndiye mfungaji wa goli la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti ametamba kuwa Stars itavuka hatua inayofuatia, mchezo huo unaanza saa 9:30 kwa saa za Rwanda na mshindi wa hapo atacheza na Uganda au Sudan Kusini