OKWI AMETUA JANA TAYARI KWA KAZI
Na Ikram Khamees. Dar es Salaam
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi amewasili nchini jana usiku majira ya saa nne akitokea kwao nchini Uganda tayari kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Ujio wa Okwi unadhihirisha kuwa Simba hawataki mchezo na wamejipanga kisawasawa kukiboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao, Okwi anajiunga na Simba kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2010 akitokea SC Villa ya nyumbani kwao Uganda.
Okwi aliuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013 na baadaye akavunja mkataba wake na kurejea tena kwao Uganda na kujiunga na SC Villa, kisha Villa wakawauzia Yanga SC kwa mkataba wa miaka miwili.
Lakini Okwi alitumikia Yanga miezi sita tu na kuvunja mkataba wake na kujiunga tena kwa mara ya pili Simba, mwaka 2015 Okwi aliuzwa tena nchini Denmark katika klabu ya Sonderjsky ambapo nako hakudumu akavunjiwa mkataba wake na kurudi tena nyumbani kwao Uganda.
Okwi akarejesha makali yake hadi kuitwa kwenye timu ya taifa ya Uganda, The Cranes kinachoshiriki michuano ya kombe la mataifa Afrika, Okwi ametua tena jana tayari kwa kujiunga na Simba SC ambapo alilakiwa na wapenzi, wanachama na mashabiki wa Simba wakiongozwa na makamu wa Rais, Geofrey Nyange "Kaburu"