Toto wamebana wameachia, Tambwe awapa ndoo ya tatu Yanga
Na Salum Fikiri Jr. Dar es Salaam
Bao lililofungwa kunako dakika ya 81 na mshambuliaji Amissi Tambwe raia wa Burundi, jioni ya leo limetosha kabisa kuwapa ubingwa wa tatu mfululizo Yanga SC dhidi ya watoto wao Toto Africans.
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ushindi wake wa 1-0 umeifanya Yanga ifikishe pointi 68 na michezo 29 sawa na vilabu vyotw vinavyoshiriki ligi hiyo.
Haikuwa kazi rahisi kwa Yanga kujipatia bao la ushindi kwani vijana wa Toto Africans "Wana Kishamapanda" leo walistahili pongezi kwa kuwabana vilivyo baba zao Yanga SC na kuwalazimisha suluhu ya 0-0 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili pia kilikuwa kigumu kwa Yanga kwani mabeki wa Toto walifanya kazi ya ziada kuwazuia washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Obrey Chirwa wasifanye madhara langoni mwao, Kipa wa Toto David Kisu leo alikuwa kikwazo kwa Yanga kwa kuokoa magoli kadhaa.
Mabadiliko yaliyofanywa na Yanga ya kumtoa Geofrey Mwashiuya na kumwingiza Emmanuel Martin viliisaidia sana Yanga kwani dakika ya 36 ya kipindi cha pili Amissi Tambwe aliipatia Yanga bao la ushindi ambalo linaelekea kuishusha daraja Toto.
Yanga watabakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Mbao FC ambao utafanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, endapo Yanga itapoteza mchezo huo bado inaweza kuwa mabingwa kwani wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa Simba SC wanaweza kuzifikia pointi 68 walizonazo Yanga lakini tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufungwa