Rufaa ya Simba FIFA utata mtupu
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa Klabu ya Simba imeshindwa kuwasilisha rufaa yake ikitaka ipewe ushindi wa mezani wa pointi tatu kutoka kwa Kagera Sugar, Simba ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Inadaiwa Kagera Sugar ilimchezesha Mohamed Faki ambaye alikuwa na kadi tatu za manjano kwa maana hiyo Simba walistahili kupewa pointi tatu na mabao mawili licha ya kipigo hicho, awali Simba ilipeleka malalamiko yake Bodi ya Ligi na ikapewa pointi tatu na mabao mawili.
Baadaye Kagera Sugar nao walikata rufaa TFF kupitia kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ambapo ikaamua kuwarudishia pointi tatu zao na mabao mawili kwa moja, pointi hizo kama Simba ingebaki nazo sasa hivi ndo wangekuwa mabingwa wa Tanzania Bara kwakuwa wangekuwa na pointi 71.
Baada ya Ligi Kuu Bara kumalizika viongozi wa Simba wakatuma Fax yao FIFA wakitaka shauri lao lisomwe upya na wao wapewe pointi tatu, lakini kwa mujibu wa FIFA, haiwezekani timu kupewa ubingwa wa mezani labda timu zipange matokeo, kwa maana hiyo rufaa ya Simba imetupwa kando na wanatakiwa kukubali matokeo