Kakolanya aitwa Stars, Dida atemwa
Na Prince Hoza. Dar es Salaam
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga amemjumuhisha kipa wa Yanga, Benno Kakolanya katika kikosi chake chenye wachezaji 23 ambacho kitaingia kambini kabla ya kuelekea Misri ambako itaenda kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Lesotho Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mayanga amemwita Kakolanya ambaye amecheza vizuri katika kikosi cha Yanga hivi karibuni na kuamua kumtema kipa mzoefu Deogratus Munishi "Dida" pia wa Yanga.
Katika orodha ya kikosi hicho cha Stars kitakachoshiriki michuano ya kombe la Cosafa itakayofanyika mwezi ujao nchini Afrika Kusini kimejumuhisha makipa wanne Aishi Manula (Azam FC) na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar.
Nyota wengine waliojumuhishwa ni Hassan Kessy, Mwinyi Haji Mngwali (Yanga), Mohamed Hussein "Tshabalala", Abdi Banda (Simba), Salim Abdallah, Agrey Morris, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni (Azam FC).
Wengine ni Himid Mao, Salum Abubakar "Sure Boy (Azam FC), Jonas Mkude, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Katika kikosi hicho pia Mayanga amewajumuhisha nyota wa kimataifa ambao ni Thomas Ulimwengu (Eskilstuna ya Sweden), Mbwana Samatta (KRC Genk ya Ubelgiji) na Farid Musa (Tenerife ya Hispania), washambuliaji hao wataungana na mzalendo Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar