Simba warejea kileleni kwa kuiduwaza Mbao CCM Kirumba
Na Paskal Beatus. Mwanza
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC jioni ya leo imefanikiwa kukomboa mabao mawili na kufunga bao la ushindi ikiiadhibu Mbao FC mabao 3-2 mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Mbao FC walitakata kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupachika bao la uongozi lililofungwa na George Sangija dakika ya 21 hali ambayo ilionekana kuwashitua Simba ambapo walilazimika kufanya mabadiliko ya haraka.
Kikosi hicho cha Mbao ambacho kilionekana kuizidi Simba kiliongeza bao la pili kupitia kwa Evarigestus Bernard dakika ya 36 akipokea pasi ya Sangija muuaji wa bao la kwanza.
Timu hizo zilienda kupumzika Simba ikiwa imelala kwa mabao hayo mawili, kipindi cha pili mpira uliendelea kuwa mgumu kwa Simba lakini walibadilika ghafla na kuweza kukomboa moja baada ya jingine yakifungwa na Muivory Coast, Fredrick Blagnon dakika ya 82 na 91.
Mzamiru Yassin akapiga bao la tatu na la ushindi ambalo likaipeleka kileleni Simba ikifikisha pointi 58 na mechi 26 na Yanga ikishuka hadi nafasi ya pili na pointi zao 56 lakini wana mechi 25