Makala: Tumuunge mkono Makonda vita ya madawa ya kulevya
Na Prince Hoza. Dar es Salaam
VITA ya kupambana na madawa ya kulevya imeshaanza na watu mbalimbalj wametajwa kuhusishwa, hatua zimeanza kuchukuliwa na wahusika wameanza kufikishwa mahakamani na wengine bado wanaendelea kuchunguzwa.
Madawa ya kulevya yameua nguvu kazi na kusababisha baadhi yao kuathilika, kwenye upande wa michezo ndio usiseme, vijana wengi wameathiliwa na dawa hizo, kwenye upande wa sanaa pia ni hivyo hivyo, kwa kifupi vijana wanateketea.
Hakukuwa na jitihada zozote za kukabiliana na wafanyabiashara wakubwa wanaoziingiza kutoka Ughaibuni, vilevile hakukuwa na jitihada zozote kuwadhibiti wafanyabiashara wanaosambaza hapa nchini.
Vijana wanazidi kuzitumia na kujikuta wakipoteza nguvu zao ambazo ziljwafanya waweze kujirafutia riziki na baadaye kujikuta hawana nguvu kabisa na kujiingiza kwenye uporaji, makundi ya vijana waliojiingiza kwenye matumizi ya mihadarati wengi wao waporaji.
Na wanafanya hivyo kwakuwa hawana uwezo wa kufanya kazi ambazo ziliwafanya wajipatie pesa, kwa maana hiyo taifa linaangamia, wachezaji nao wakawa wanaathiliwa na dawa hizo na kujikuta wakipoteza viwango vyao.
Tumeshuhudia wachezaji kadhaa hapa nchini wakijihusisha moja kwa moja na matumizi ya madawa ya kulevya na pia wakapoteza viwango vyao, sipo hapa kutaja majina ya wachezaji hao lakini wengi wao wanafahamika lakini siwezi kumtaja mmoja mmoja.
Madawa ya kulevya ni pamoja na "Unga", Bangi na Mirungi, Unga umegawanywa makundi mbalimbali kulingana na thamani yake, kuna Cocaine, Heroin na nyinginezo, lakini Bangi na Mirungi ni aina moja tu ya majani ambayo yanatajwa kuwa ni hatari kwa afya ya mtumiaji.
Wasanii nao wengi wao wamepoteza vipaji vyao kutokana na kutumia dawa hizo, na kwa bahati mbaya wengineo walipoteza maisha, msanii Langa aliyetamba na kundi la Wakilisha lililokuwa na wasanii watatu, yeye, Sarah na Witness, alifariki dunia na kifo chake kilitajwa kuwa kimetokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Ukiachana na Langa, msanii mwingine aliyefariki kwa dawa za kulevya ni Mangwea, msanii huyo alifia nchini Afrika Kusini na inasemekana kabla ya kuanza safari alitumia dawa hizo, na zipo baadhi ya Clip za video zilizoonyesha madaktari wa nchini Afrika Kusini wakiufanyia upasuaji mwili wa msanii huyo uliokuwa na dawa nyingi za kulevya ambazo alizimeza ilj azilete Tanzania.
Wasanii wanatajwa kubeba dawa za kulevya na wapo waliokamatwa ndani na nje ya nchi, pia wapo wasanii wanaotumia dawa hizo, Ray C mmoja wa wasanii waliotikisa kwenye muziki lakini akapoteza kipaji chake kwa kutumia dawa hizo, kwa sasa Ray C si yule wa miaka ile.
Daz Baba ambaye naye alitamba kwenye kundi la Daz Nundaz lililotikisa naye ameangamia kwa dawa za kulevya, Daz kwa sasa ni muathilika wa dawa hizo, ukiachana na Daz, Chid Benz rapa aliyeibuka kwa kasi ya ajabu akiwa na sauti nene naye ameangamia kwa dawa hizo.
Chid Benz aliyetamba na wimbo wa Darisalaam Stand Up, kwa sasa ni muathilika wa dawa hizo, T.I.D naye alijiingiza kwenye matumizi hayo na kujikuta anapoteza sauti yake tamu aliyotamba nayo kwenye wimbo wa Zeze, wasanii wetu wanaangamia.
Lakini inasemekana kuwa wasanii hao hao wamekuwa wakishiriki kusambaza dawa hizo kwa wenzao, wasanii wanaotajwa kuwauzia wenzao ni Dogo Hamidu, Mr Blue, Wema Sepetu na wengineo ambao wamejumlishwa kwenye majina 65 yaliyotangazwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Poul Makonda.
Makonda ameamua kupambana na madawa ya kulevya na tayari watu kadhaa wameshahojiwa na Jeshi la Polisi, Makonda hakusita kuwataja wafanyabiashara wakubwa wanaodili na dawa hizo mpaka kuleta tafrani kwa wananchi ambao wameanza kumshutumu.
Makonda ametaja majina makubwa ambayo ndani yao wamo viongozi wa kisiasa, dini na soka, lakini nguvu inapaswa kuongezeka kwa Makonda ili kumuunga mkono kwenye sakata hili, asibaki peke yake kwani tumeshapoteza wasanii wengi na wanamichezo ambao wangetuletea sifa kubwa kwenye taifa letu.
Lakini pia vijana wengi wameangamia kwa dawa za kulevya na kujikuta wakijiingiza kwenye uharifu mwingine kama wa uporaji, maisha yetu huko mtaani yamekuwa ya shida, kama umevaa vito vya thamani ujue uko shakani kwani "Mateja" wakikuona kwao ni furaha.
Wanaamini wakikubana watapata hela ya kununulia 'Unga', nimeshawahi kumuona "Teja" akishiriki kujiibia yeye mwenyewe ili akapate unga japo kidogo kwani alikuwa alosto kama wenyewe wanavyoita, mteja huyo aling' oa mabati ya nyumba yake ya urithi na kwenda kuuza
Tuungane na Makonda kwenye vita hii na tuache ushabiki kwa wale wanaotajwa, tusiwaamini sana watu waliojichomeka kwenye siasa, michezo na dini, inawezekana waliotajwa ni walengwa tosha ila kelele za kuwatetea ni nyingi mno
ALAMSIKI