Makala: Chakori ni funzo kwa wasanii wetu, wabadilike
Na Prince Hoza. Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii Mhe Nape Moses Nnauye majuzi alipiga marufuku uingizwaji na usambazwaji wa filamu za kigeni kwa vile zinaua soko la filamu za ndani.
Hii yote imetokea baada ya filamu za Kitanzania maarufu Bongomovie kukosa soko, Wapenzi wa filamu nchini hawanunui tena filamu za hapa na wamekuwa wakitazama filamu za kigeni.
Kwa maana hiyo wasanii wetu nchini wanakosa pesa za kuendesha maisha yao na kujikuta wakijitumbukiza kwenye skendo, hakuna mtu anayemfuatilia JB, Ray au Wema Sepetu, wala hakuna mtu anayemfuafilia Jengua, Irene Uwoya wala Johari, kwa kifupi wasanii wetu wamepoteza mvuto wa kibiashara tangu alipotutoka Steven Kanumba.
Waziri Nape mbali ya kuzipiga stop filamu za nje, pia aliwataka wale wafanyabiashara wa maeneo ya Kariakoo hasa mitaa ya Agrey, Kongo na Msimbazi ambako ndiko inakofanyika biashara ya usambazaji wa filamu hizo kuacha mara moja mpaka pale utaratibu utakapopangwa.
Inasemekana filamu za nje hazilipi kodi, nyingi zimekuwa zikipatikana kwa njia ya Kudownload kupitia mitandao, hali ya soko la filamu zetu limezidi kushuka, wasanii wanalia kila kukicha kuwa maisha magumu, yaani hawauzi, na Mhe Nape amesikia kilio chao na kuamua kuziondoa sokoni muvi za nje.
Filamu za Kinigeria, Amerika, Uchina na Uhindi zimekuwa zikifanya vizuri sokoni na kuliangamiza kabjsa soko la filamu za ndani, watu hawana mpango tena na JB, watu hawataki kumsikia tena Wema Sepetu na ndio maana wasanii wetu wamekuwa wakifanya biashara haramu kwakuwa biashara halali hailipi, Wema ukitaka kumuona nenda Central ana kesi ya madawa inamsumbua.
KIPI KIMEWAANGUSHA?
Ukiangalia kwa haraka unaweza kusema kilichowaangusha ni anguko la uchumi hapa nchini mwetu na watu kukosa pesa za kununua kazi zao, siyo siri bei ya filamu zetu ziko juu kuliko zile za kigeni, hivyo watu wengi wameamua kununua filamu za kigeni.
Lakini kiundani kabisa kilichowaangusha wasanii wetu ni kuiga tamaduni za Kimagharibi, wengi wamechoshwa na mambo ya kuiga wazungu, Wasanii wetu badala ya kuutangaza utamaduni wa Kitanzania wamejikuta wakitangaza tamaduni za Kizungu.
Hapo wamejikuta wakipotosha jamii badala ya kuielimisha, wasanii wetu wamejikuta wakiiharibu jamii ya Kitanzania, watoto wetu wanaiga kupitia filamu hizo hizo ambapo nao wamekuwa wakivaa kama akina Wema Sepetu au Irene Uwoya, wasichana ndio wameharibika kabisa maana wanatembea uchi barabarani.
Ni aibu hata kuongozana nao maana utadhalilika, vijana wa kiume nao wamekuwa wakivaa mlegezo jambo ambalo ni hatari kwao, hizo ndio filamu zetu za ndani ambazo Mhe Nape ameamua kuzitetea, kiukweli Nape alipaswa kuwaambia ukweli tu kuwa kazi zetu hazifai na wajikite kwenye uhalisia wa tamaduni zetu.
Nimekuwa mpenzi mkubwa wa kutazama filamu za kigeni hasa ya Kihindi, na sasa nafuatilia vema 'Season' ya Udaan ambapo ndani yake yupo Chakor ambaye anaibeba Season hiyo, kwakweli Mhe Nape naye alipaswa kuitazama season hiyo kisha angewaambia ukweli wasanii wetu waige kitu kutoka kwenye season hiyo badala ya kuifungia.
Season hiyo inafundisha, inaelimisha na inaburudisha, pia sijaona sehemu inayopotosha jamii, hizo ndio kazi nzuri ambazo zilipaswa kufanywa na wasanii wetu ambao wamejikuta wakishiriki kuharibu kizazi chetu, season ya Udaan inapendwa hata na watoto wadogo kwani imekuwa rafiki na watu wote.
Nasikia na hiyo nayo imezuiwa na Nape, namuomba Mheshimiwa Nape awaambie ukweli wasanji wetu kuwa Watanzania hasa watazamaji wa filamu tunataka tamaduni zetu zionekane kama ilivyo kwa wenzetu wa India ambao wamekuwa wakituonyesha tamaduni zao, Mwisho namalizia kwa kusema Hili filamu za Kibongo zitawale soko zinahitaji akili na maarifa ya ziada ama sivyo tutazipiga kumbo kabisa