Yanga yavunja mwiko Songea, yaigagadua Majimaji 1-0 na kuisogelea Simba kileleni
Na Salum Fikiri Jr, Songea
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Dar Young Africans maarufu Yanga, jioni ya leo imejiongezea pointi tatu baada ya kuilaza Majimaji bao 1-0 mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Mchezo ulikuwa mkali na wa kusisimua huku wenyeji Majimaji wakiliandama lango la Yanga kama nyuki na kama si uimara wa mabeki wa Yanga na kipa wao huenda matokeo yangekuwa mengine.
Yanga walitangulia kupata bao la mapema kabisa likifungwa na Deus Kaseke, hata hivyo Yanga nao watajilaumu kufuatia washambuliaji wake kutokuwa makini, kwa ushindi huo wa leo Yanga imevunja mwiko wa kutoifunga Majimaji kwenye uwanja wa nyumbani kwao tangu mwaka 1985.
Yanga pia imeamsha mbio za kuifukuza Simba kileleni kwani imefikisha pointi 43 ikiwa nyuma ya pointi moja na Simba inayoongoza Ligi hiyo, Simba kesho itacheza na Mtibwa Sugar uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro