David Burhan afariki dunia
Na Prince Hoza, Dar es Salaam
Kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/14, David Abdallah Burhan amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Bugando, Mwanza.
Kipa huyo wa Kagera Sugar ya Bukoba alifikishwa hospitalini hapo jana kutoka Bukoba na kwa bahati mbaya asubuhi ya leo ameaga dunia.
Nahodha wa Kagera Sugar George Kavila ameiambia Mambo Uwanjani kwamba Burhan mtoto huyo wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Pan Africans, Abdallah Burhan alikuwa anasumbuliwa na tumbo la kuhara.
Kavila amesema matatizo hayo yalianza wakati wamekwenda Singida kucheza na wenyeji wao Singida United mechi ya Kombe la Shirikisho la soka Tanzania (TFF) maarufu kama kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) katikati ya wiki.
Uongozi wa Kagera Sugar ulijitahidi kuhakikisha Burhan anapona haraka kwani ulimkodia ndege na kumsafirisha Bukoba ambako nako walimpeleka Bugando na akafikwa na mauti, mwilj wa marehemu utasafirishwa hadi Iringa kwa mazishi, marehemu aliacha mke na watoto wawili