Smart Sport yaibwaga TFF Mahakamani
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, jana imeipa ushindi kampuni ya kuuza na kusambaza vifaa vya michezo ya Smart Sport ambayo ilifungua kesi ya madai dhidi ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF).
Kwa mujibu wa Mahakama hiyo, TFF imetakiwa kuilipa Smart Sport Shilingi Milioni 30 za Kitanzania zikiwa kama gharama zitokanazo na deni la kampuni hiyo dhidi yao.
Awali TFF kupitia kwa Afisa Habari wake Alfred Lucas alikanusha vikali TFF kudaiwa na Smart Sport, lakini Mahakama ikaona TFF inadaiwa na kampuni hiyo.
Smart Sport inaidai TFF baada ya kugharamia vifaa vya michezo ikiwemo jezi, viatu, soksi, mipira, tracksult na vinginevyo kwenye timu zote za taifa na imekuwa ikipigwa danadana kila inapodai fedha zake.
Mtandao huu ulipomuuliza Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Emily Malinzi kuzungumzia sakata hilo alishindwa kutoa maelezo na kudai hana muda kwa sasa kuelezea suala hilo na labda wamtafute siku nyingine.
Hata hivyo TFF inaweza kukata rufaa ndani ya siku 30 kupinga ushindi iliopewa Smart Sport wa kutakiwa kulipwa milioni 30