STAA WETU: DEOGRATUS MUNISHI 'DIDA', SHUJAA WA YANGA NA TANZANIA KWA UJUMLA
Na Exipedito Mataruma, DAR ES SALAAM
MACHO yake yalikuwa makini kuitazana penalti iliyopigwa dakika ya 87 zikisalia dakika tatu mpira kumalizika, si mwingine ni Deogratus Boniventure Munishi maarufu kama Dida akifananishwa na kipa wa Brazil Nelson Dida.
Dida alikuwa shujaa Jumatano iliyopita ikifanikiwa kuiondosha mashindanoni GD Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, Yanga ilishinda magoli 2-0 Uwanja wa Taifa Dar es Salaam shukrani kwa Simon Msuva na Matheo Antony waliofunga mabao safi kabisa.
Yanga ilifungwa bao 1-0 katika Uwanja wa Esparanca mjini Dundo Angola goli lililofungwa na mkongwe Love Caburunca, matokeo hayo yameivusha Yanga hadi hatua ya makundi kombe la Shirikisho barani Afrika ikiwa ni historia katika ukanda wa Afrika mashariki.
Yanga inakuwa timu ya kwanza ya nchini kufikia hatua hiyo, pia ikumbukwe Yanga iliwahi kufanya hivyo mwaka 1998 ilipotinga makundi ligi ya mabingwa barani Afrika.
ALIFIKAJE YANGA!
Dida alianza kuchomoza akiwa na Manyema ya Ilala ambako ndiko kulikochangia mafanikio yake, Dida alichagua nafasi ya kipa badala ya nafasi nyingine za uwanjani hasa kutokana na urefu alionao ulimfanya haweze kucheza mipira ya juu.
Dida alifanya vizuri na Manyema mpaka uongozi wa Simba ukaamua kumchukua, Dida na Bakari Kigodeko ndio wachezaji pekee wa Manyema waliosajiliwa na Simba, kipa huyo alisajiliwa Simba hasa baada ya kuachana na kipa wake Amani Simba.
Kipa huyo alikutana na makipa wazoefu Juma Kaseja na Ali Mustafa 'Barthez' ambao hata hivyo hakuwaogopa, Dida alijiunga na Simba mwaka 2008 na mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Villa Squad Simba ikishinda 4-1 na uliofuata dhidi ya Polisi Dodoma ukiisha kwa sare ya 2-2.
Anasema alipata unafuu wa kupata namba Simba hasa baada ya Juma Kaseja kuhamia Yanga, Dida aliyezaliwa mwaka 1989 Moshi, Mkoani Kilimanjaro katika familia ya mzee Boniventure Munishi na mama Hilda Temu akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo ya watoto wanne, nduguze ni Ismail, Kasija na George.
Alisoma Madenge shule ya msingi kuanzia mwaka 1996 mpaka 2002 kisha kujiunga na Makongo Sekondari mwaka uliofuatia lakini alisoma kwa mwezi mmoja tu na kujikita katika soka, alianza kucheza soka mwaka 1993 katika viwanja vya Temeke msikiti wa Tungi.
Dida alijiunga na timu ya Temeke Kids nwaka 2000 iliyokuwa chinj ya kocha Tunge na kufanya mazoezi katika viwanja vilivyokuwepo jirani ya uwanja wa Taifa wa zamani (Sehemu hiyo sasa uwanja mkuu wa Taifa).
Mwaka 2004 alisajiliwa na Coastal Union ya Tanga na kucheza Ligi Daraja la kwanza, mwaka uliofuata alijiunga na timu ya Chuoni ya Zanzibar iliyokuwa inashiriki ligi Daraja la kwanza visiwanj humo.
Mwaka uliofuata alijiengua na kurudi Dar es Salaam na kuendelea kujifua katika viwanja vya Tungi Temeke, Februali 2007 alijiunga na Makondeko ya Temeke lakini Machi mwaka huo huo alijiunga na Mkunguni ya Ilaka kushiriki ligi Daraja la tatu.
Hapo hakukaa sana kwanj Aprili 2007 alijiunga na Manyema na kufanikiwa kuipandisha ligi kuu bara, Manyema ndiyo timu iliyomfungulia milango Dida kuzichezea klabu kubwa nchini za Simba Sc, Mtibwa Sugar, Azam Fc na sasa Yanga Sc pia akiitwa Taifa Stars.
Dida ameweza kuipa ubingwa wa bara Yanga mara mbili mfululizo huku pia akifanikiwa kuiwezesha kuingia fainali kombe la Azam Sports Federation Cup maarufu FA Cup ambapo Jumatano ijayo watacheza fainali na Azam Fc.