MAONI: KAULI ZAKO HANSPOPPE ZINAWACHOSHA WANASIMBA

Na Prince Hoza, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Kamati ya usajili wa klabu ya Simba Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Zacharia Hanspoppe amekuwa na majibu ya kuudhi na kukera wapenzi na mashabiki wa Simba.

Kuna wakati najiuliza kati ya yeye na wapenzi na mashabiki wa Simba nani hasa wenye uchungu pale timu ibapotokea imefanya vibaya, Hanspoppe anashindwa kuwa na kauli nzuri kwa Wanasimba hasa wapenzi wanapotaka kupewa matumaini.

Hanspoppe chini ya kamati hiyo bdiyo imekuwa ikihusika kusajili na kuacha wachezaji, mwenyewe anadai ni mapendekezo ya kocha, lakini kimtazamo si kweli, Kocha anatoaje mapendekezo wakati hayupo.

Simba itaingia msimu ujao bila kocha huyu wa sasa, kila msimu Simba imekuwa ikianza na mwalimu mpya, kuna mipango imeandaliwa ya kumtosa Jackson Mayanja na tayari mchakato wa kuajili kocha mpya umeshaanza.

Muda wowote Simba itamtangaza kocha mpya na anatajwa Milovan Cirkovic raia wa Serbia, pia Bobby William raia wa Ubelgiji naye yumo kwenye rada hizo, kwa maana hiyo Mayanja hawezi kutoa mapendekezo yake na yakaheshimika.

Kwa vyovyote Hanspoppe atafanya usajili pasipo kuhusisha benchi la ufundi, atarudia yaleyale, Hanspoppe amehudumu kama mwenyekiti wa kamati hiyo miaka minne sasa na yote hiyo haijaonya ubingwa wa bara wala nafasi ya pili.

Ni aibu iliyoje, Wanachama wa Simba wanalilia mafanikio, wanataka timu yao apewe Mo yaani Mohamed Dewji mfanyabiashara maarufu nchini, Mo anaitaka Simba ili ailetee mafanikio kama ilivyokuwa zamani.

Akina Hanspoppe na wenzake wanaonekana wasanii yaani wapiga dili kama vijana wa kileo wanavyotamka, tangia walipoichukua timu toka mikononi mwa Alhaj Ismail Aden Rage hakuna walichofanya zaidi ya blaa blaa.

Simba kila msimu inafumuliwa upya, na kila kocha anayekabidhiwa anasema kikosi kinahitaji muda ili kuzoeana, kwahiyo kila mwaka Simba inahitaji mazoea, baada ya kuvurunda kwenye msimu uliomalizika jana Jumapili Simba ikikamata nafasi ya tatu na pointi 62 tena ikichapwa 2-1 na JKT Ruvu, mashabiki wanataka kauli thabiti ili kujua mwenendo wa timu yao.

Lakini Hanspoppe ameshawahi kuelezea kuhusu mwenendo wa Sinba na akawaangushia lawama wachezaji na baadaye mashabiki, kauli zake haziingii akilini hata kidogo, Hanspoppe ameonekana akimshushia lawama wachezaji Hassan Kessy na Ibrahim Hajibu na hawapishani sana na Rais wa Simba Evans Aveva.

Hanspoppe atambue kwamba Simba si mali ya viongozi bali ni ya wanachama na mashabiki ambao ndio wanaokerwa na maneno ya kebehi toka kwa mahasimu zao Yanga, Mashabiki wa Simba wanakutana na majina ya utani kama 'Vyura', 'Wamatopeni' na 'Wamchangani'.

Lakini bado Hanspoppe anashindwa kuwatuliza kwa kauli nzuri, kiongozi huyo amejikuta akinusurika kichapo toka kwa mashabiki wenye hasira baada ya majibu yake ya nyodo, sioni uongozi wa namna hii, sioni kiongozi anakuwa na jeuri za namna hii eti ti ana pesa za kumwaga.

Lakini haelewe Wanasimba wanahitaji furaha, hawajazoea kukerwa, wamezoea ushindi kila siku, suala la kufungwa kwao ni maumivu tena kuliko yale ya kuumizwa na kitu chenye ncha kali, kikubwa anachopaswa kukifanya Hanspoppe ni kukubali kwamba Wanasimba ndio wenye timu yao na yeye ni mtumishi tu, asijione kama mfalme.

Tuonane wiki ijayo. Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa michezo na burudani hapa nchini anapatikana kwa namba 0652626627

Zacharia Hanspoppe

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA