ANAYEKUMBUKWA: PATRICK MAFISANGO, INJINI YA SIMBA ILIYOZIMIKA GHAFLA
Na Mrisho Hassan, DAR ES SALAAM
SIMBA SC inahaha kusaka kiungo mchezeshaji mwenye uwezo wa hali juu kama ilivyokuwa kwa Patrick Mutesa Mafisango (Sasa Marehemu.
Marehemu Mafisango alikuwa na kiwango kizuri na aliwakosha wengi hasa mashabiki wa Simba Sc, jamaa alikuwa na uwezo wa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi kwa wenzake.
Pengo lake halitazibika kamwe kwani alifariki katika ajali mbaya ya gari iliyotokea Mei 17 mwaka 2012 maeneo ya Chang' ombe Dar es Salaam.
Mchezaji huyo ndio kwanza alirejea na wenzake nchini wakitokea Sudan walikokwenda kushiriki mchezo wao wa kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya 16 bora na Al Shandy ambapo Simba iliondoshwa kwa mikwaju ya penalti 8-7.
Mafisango ni kati ya wafungaji hodari na alikuwa akiibeba Simba pale ibapoyumba, uwepo wake ulitengeneza kombinesheni kali ya Felix Sunzu na Emmanuel Okwi ambayo ilikuwa haikamatiki.
Alizaliwa Machi 9, 1980 huko DRC na alibahatika kuzichezea timu mbalimbali katika maisha yake ya soka, alichukua uraia wa Rwanda badala ya nchi yake ya DRC lakini alizikwa DRC.
Marehemu alianza kuichezea APR ya Rwanda kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2007 alipojiunga na Atraco kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2009, alirejea tena APR mwaka 2009 hadi 2010 alipojiunga na Azam Fc ya Tanzania aliyodumu nayo hadi mwaka 2011 na kujiunga na Simba ambapo alicheza hadi 2012 umauti ulipomfika.
Enzi za uhai wake Mafisango alikuwa akicheza kama kiungo mchezeshaji na alikuwa rafiki mkubwa na kiungo wa Yanga Mnyarwanda Haruna Niyonzima, lakini nyota huyo alibadili namba alipokuwa Azam ambapo alicheza kama sentahafu.
Maisha ya Azam yalikuwa magumu kwake ikabidi abadilishwe Simba na Ramadhan Chombo 'Redondo' ambaye alikuwa katika kiwango cha juu, Mafisango akiwa Simba alitamba na kuwafanya mashabiki wa Simba kutembea vifua mbele.
Mafisango anakumbukwa vema kwenye ushindi wa mabao 5-0 ilioupata Simba dhidi ya mahasimu wao wakuu Yanga Sc uwanja wa Taifa Dar es Salaam mchezo wa ligi kuu bara, katika mchezo huo Mafisango aliwahenyesha vilivyo Yanga na kuacha gumzo hadi leo