ANAYEKUMBUKWA: JUMA NASSORO PONDAMALI "MENSAH", ALIKUWA KIPA NWENYE VITUKO LANGONI
Na Prince Hoza, DAR ES SALAAM
KATIKA historia ya magolikipa hapa nchini wapo wengi kama vile Peter Manyika (Senior), Chachala Muya, Kichochi Lemba, Abdul Kipyenga, Spear Mbwembwe, Issa Manofu na wengineo ambao walitaka kumuiga Juma Pondamali 'Mensah' kwa vituko na mbwembwe zake akiwa langoni, lakini hawakumfikia hata robo yake.
Pondamali alikuwa ni wa aina ya kipekee ndani ya nchi hii ambaye kwa sasa ndiyo anawanoa makipa takribani wote wa mabingwa wa soka Tanzania bara Yanga Sc inayonolewa na Mholanzi Hans Van der Pluijm na msaidizi wake Juma Mwambusi.
Achana na yote, Pondamali anashikilia rekodi ya utukutu, kipa huyo alifungiwa mara tano, na pia mara nne mapambano yalivunjika, Pondamali alizaliwa mwaka 1957 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Ocean Road.
Pondamali alipata masomo yake akianzia shule ya msingi Mlimani na baadaye Karume kabla ya elimu yake ya sekondari kuipata Mzizima muda wote huo wa utoto wake soka likiwa ndani ya damu yake.
KOCHA MZUNGU AMWIBUA JANGWANI
Kocha raia wa Romania Victor Stanculescu mwanzoni mwa miaka ya 70 baada ya kuona wachezaji wa Yanga umri wao unasogea aliita watoto wenye vipaji wenye umri wa Kids yaani miaka 14/15 ili waje wachukue nafasi za wakongwe.
Na ndipo walipojitokeza watoto takribani mia na kupatikana wachache akina Mohamed Mkweche, Adolf Richard, Kassim Manara, Mohamed Tostao, Gordian Mapango, Juma Pondamali na wengineo ambao kwa maelezo ya Victor aliwatabiria kuwa wote lazima watacheza timu ya taifa na ndicho hatimaye kilitokea.
Pondanali na wenzake walipandishwa hadi kikosi cha pili na baadaye mwaka 1974 walipandishwa hadi kikosi cha kwanza na Pondamali akiwa kipa wa tatu akifuatiwa na Muhidin Fadhil na Elias Michael na kutengeneza mziki mzito ndani ya vijana wa Jangwani na walifanya vizuri mwaka 1974 kwa kuwafunga mahasimu zao Simba.
Mwaka uliofuatiwa wakachukua ubingwa wa Klabu bingwa Afrika mashariki na kati na balaa likitokea katika mashindano ya Klabu bingwa Afrika na kutolewa na Enugu Rangers ya Nigeria.
YANGA YAMEGUKA NA KUUNDWA PAN AFRICAN
Matatizo ya wanachama kufuata mkumbo na kutopima mambo, wakamsikiliza kocha Mzaire Tambwe Leya na kuwapuuza wachezaji kwa kila jambo ambalo Tambwe aliwaambia baada ya ile mechi ya kwanza kule Nigeria kutoka sare, Kocha aliapa kuwa ni lazima wataiondosha katika mashindano Enugu na baada ya kutolewa akashusha lawama kwa wachezaji.
Tambwe Leya aliwalaumu akina Boy Idd, Sunday Manara, Omary Kapera, Gibson Sembuli kuwa wameihujumu timu kwahiyo wanachama waamue moja atoke yeye au wachezaji na ndipo wachezaji walipoamua kutimka kwa kuzingatia kuwa hawakuona kosa lao.
Wakubwa wote wakaenda kuunda timu inayoitwa Nyota Afrika ya Morogoro na wale waliokuwa watoto wakajiunga na Pilsner ya Dar es Salaam na baada ya mwaka akina Sembuli wakarudi kuungana na vijana wao ambao ndio walikuwa moto wa kuotea mbali na kuunda Pan Africans kwa masharti kuwa wote vijana wapewe ajira, na kweli vijana wote waliajiliwa kwenye kiwanda cha madawa hivyo ndivyo ilivyounda Pan ikiwa chini ya mzee Tabu Mangala na Shiraz Sharif.
MTUKUTU AKIWA UWANJANI, MPOLE AKIWA NJE YA UWANJA.
Kama kuna watu waliokuwa wakorofi ndani ya uwanja na wapole nje ya uwanja basi Juma Pondamali alikuwa habari nyingine, hawa akina Haruna Moshi 'Boban', Juma Nyosso, Juma Kaseja na wengineo wanasingiziwa tu.
Pondamali aliwahi kufungisha goli kwa makusudi halafu akasimama kumsubiria beki mkorofi Fred Minziro enzi hizo akiwa nahodha wa Yanga, Minziro alionekana akilalanimika lakini hakuweza kumfikia Pondamali kwani angeweza kuchapwa makonde , kipa huyo alikuwa mwanakareti mzuri.
Pondamali ndiye kipa pekee hadi sasa mwenye historia ya kucheza fainali za mataifa Afrika mwaka 1981 nchini Nigeria.
Yapo mengi yanayomuhusu kipa huyo ila sitaweza kuyaeleza yote leo tusubiri siku nyingine kama hii ya leo