STAA WETU: JUMA ABDUL JAFFARI, MPISHI WA GOLI LA NGOMA, WAARABU WAMZIMIA
Na Exipedito Mataruma, ALIYEKUWA MISRI.
JUMA Abdul Jaffari ukiongeza lingine Mnyamani ni jina linalochomoza kwa sasa kwenye medani ya soka hapa nchini na kwingineko.
Anacheza nafasi ya ulinzi wa pembenj hasa akimudu upande wa kulia na akisaidia kupandisha mashambulizi, Abdul amekuwa na uwezo mkubwa wa kusababisha mashambulizi na timu yake kung' ara.
Akiwa katika kikosi hicho cha mabingwa wa soka nchini Yanga Sc, Abdul ameisaidia hadi kukamata usukani wa ligi kuu na kuweka hai matumaini yake ya kutetea ubingwa wa bara.
Nyota huyo pia amekuwa mpigaji mzuri wa mipira iliyokufa kwa maaba faulo, Abdul amejaaliwa nguvu za miguu na amekuwa akipiga mashuti makali hatimaye kuifungia timu yake magoli.
Anakumbukwa kwa magoli yake ya mashuti moja dhidi ya Azam Fc, ambapo alisawazisha makosa yake baada ya kujifunga kisha akapanda na kupiga bunduki kali na kufunga la kusawazisha, katika mchezo huo timu hizo zenye ushindani zilifungana mabao 2-2.
Abdul pia akafunga bao lingine dhidi ya APR ya Rwanda mchezo wa ligi ya mabingwa uliofanyika mjini Kigali ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1, goli lake likiisaidia kuivusha Yanga raundi ya pili ya michuano hiyo mikubwa na yenye ukwasi mkubwa wa fedha.
Nyota yake inazidi kung' ara licha kwamba kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars Charles Boniface Mkwassa ameshindwa kumuona, Mkwassa amekuwa akimtumia zaidi Shomari Kapombe.
Lakini Abdul ni mmoja kati ya wachezaji bora kwa sasa Afrika mashariki, beki huyo amekuwa katika kiwango cha juu mno na kuipa nguvu Yanga, Abdul alisajiliwa na Yanga misimu mitatu iliyopita akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo yenyewe ilimchukua toka Toto Africans ya Mwanza.
Tayari beki huyo ameshampoteza kabisa Mnyarwanda Mbuyu Twite ambaye alikuwa akianzishwa namba mbili, kasi ya Abdul imemfanya kocha wa Yanga Mholanzi Hans Van der Pluijm kumchezesha namba sita au tano.
WAARABU WAMTAMANI
Juma Abdul aliwashangaza Waarabu hasa wakati timu yake ya Yanga ilipocheza na Al Ahly mchezo wa marudiano ligi ya mabingwa barani Afrika hatua ya 16 bora uliofanyika uwanja wa Borg Al Arab mjini Alexandria.
Kwa bahati nzuri niliushuhudia kwa macho yangu kwa maana nilikuwepo uwanjani, Abdul ndiye mpishi wa bao la Yanga walilokipata dakika ya 57 lililofungwa na Mzimbabwe Donald Ngoma, lilikuwa goli zuri lakini lilitokana na jitihada binafsi za Abdul.
Mara baada ya kumalizika mchezo huo, mashabiki wa soka nchini Misri walifurahishwa naye huku wengine wakizitaka timu za Misri kumchukua.
Abdul alizaliwa Novemba 10 mwaka 1992 mjini Mwananyamala Dar es Salaam na kuanza soka utotoni, nyota yake ilianza kuonekana tangia anacheza chandimu, Malengo yake ya baadaye mara baada ya kuachana na Yanga ni kucheza soka la kulipwa ughaibuni.
Yanga wameshamuongezea mkataba mpya wa miaka miwili utakaomalizika mwaka 2018