SIMBA HAOOOO ZANZIBAR KUIWINDA AZAM MEI MOSI
Na Salum Fikiri Jr, ZANZIBAR
SIMBA SC imewasili Zanzibar jioni ya leo ikitokea jijini Dar es Salaam ikiwa tayari kabisa kuiwinda Azam Fc mchezo wa ligi kuu bara Mei mosi mwaka huu uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Simba ikiwa na mechi ngumu hutumia kambi ya Zenji kujiwinda zaidi, mchezo wake na Azam utakuwa mkali kutokana na kila timu kutaka kumaliza kwenye nafasi za juu.
Klabu hiyo yenye maskani yake mtaa Msimbazi ina pointi 57 na mechi 25 ikikamata nafasi ya pili nyuma ya Yanga inayoongoza ikiwa na pointi 59 lakini imecheza mechi 24, Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa imecheza mechi 24.
Meneja wa Simba Abbas Ally amesema vijana wake watakuwa imara zaidi wakiwa Zanzibar kwani kuna utulivu wa hali ya juu tofauti na Dar es Salaam, Ally amewataka mashabiki wa Simba kuwa watulivu katika kipindi hiki na ushindi utapatikana tu.
Simba ilipoteza mechi mbili mfululizo moja ikifungwa na Coastal Union mabao 2-1 mchezo wa Robo fainali kombe la FA na nyingine ilifungwa na Toto Africans mchezo wa ligi kuu bara zote zikipigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam