MAONI: HAYA YOTE WAMEYATAKA TFF YA MALINZI, NUSU FAINALI YA FA CUP KUCHEZWA "UCHOCHORONI"

Na Prince Hoza, DAR ES SALAAM

KAMA ingetokea mwamuzi aliyechezesha pambano la kombe la Azam Sports Federation Cup maarufu FA Cup Nusu fainali kati ya Yanga Sc na Coastal Union uliofanyika uwanja wa Mkwakwani Tanga angepoteza maisha basi lawama zote zinngeelekezwa TFFna rais wake Jamal Malinzi kwa kupeleka mechi hiyo "Uchochoroni".

Mechi hiyo yenye uzito wake ilipaswa kuchezwa uwanja mkuu wa Taifa, mechi ya Nusu fainali inahitaji usalama wa kutosha lakini kwa jana ni kichekesho tupu.

Pambano kati ya Yanga na Coastal lilivunjika kunako sakika ya 110, ina maana zilisalia dakika kumi kumalizika mchezo huo huku Yanga Sc ikiwa mbele kwa mabao 2-1, mashabiki wa Coastal Union walianza vurugu kwa kurusha mawe uwanjani na kusababisha wachezaji wa Yanga kutoka nje kuogopa kuumia.

Mwamuzi namba mbili Charles Simon alijeruhiwa vibaya maeneo ya usoni na kupelekea kupatiwa matibabu ya haraka, mbali na kuumia vurugu hizo zilisababisha pambano hilo kuvunjika na kuwaacha watu wengi na mshangao.

Sheria za FIFA ziko wazi timu iliyofanya vurugu itatolewa mashindanoni  na mashabiki waliovunja pambano ni wa Coastal Union kwani timu zilizokuwa zikicheza jana ni hizo Yanga na Coastal.

Inadaiwa chanzo cha vurugu hizo ni mwamuzi wa kati wa mchezo huo Abdallah Kambuzi kuyakubali magoli mawili ya Yanga ambayo inasemekana hayakuwa ya halali, goli la kwanza alifunga Donald Ngoma, Ngoma inadaiwa alikuwa ameotea.

Aidha mwamuzi huyo alikubali goli la pili la Yanga lililofungwa na Mrundi Amissi Tambwe, goli hilo inadaiwa alifunga kwa mkono, ina maana mwamuzi huyo pamoja na wale wa pembeni waliingia na matokeo uwanjani.

Hilo sina uhakika nalo lakini kiukweli kabisa matokeo ya uwanjani yaheshimike, na refa ndiyo mwamuzi wa mwisho, kama kuna timu inaona ilionewa inaweza kuwasilisha malalamiko yake TFF na hatua za kinidhamu zikachukuliwa na mwamuzi akaadhibiwa.

Si mara ya kwanza waamuzi kuadhibiwa na TFF, nasema hivyo kwa sababu sheria ikivunjwa hatua huchukuliwa haraka, hakuna kifungu chochote cha sheria si hapa wala duniani kwa ujumla inayohalalisha mkosaji ahukumiwe papopapo, ndiyo maana zikawepo mahakama.

Mwamuzi wa mchezo wa jana alifanya makosa kuibeba Yanga basi viongozi wa Coastal wangefanya hayo, kwa maana hiyo sasa tukirudi kwenye sheria, Yanga inastahili kusonga mbele kwa ushindi wake wa jana wa mabao 2-1.

Coastal imeponzwa na mashabiki wake na inapaswa kuadhibiwa, mara kwa mara TFF imekuwa ikisisitiza uhuni viwanjani hautakiwi, mashabiki wakorofi wanaziponza vilabu na kupelekea kutozwa faini.

Diego Armando Maradona aliwahi kufunga goli la mkono na likaivusha timu yake ya taifa ya Argentina, mwamuzi akuona na akanyoosha kati, Waingereza hadi leo wanamchukia Maradonna kwa goli hilo, achana na Maradonna, Madaraka Seleman "Kiminyio" aliwahi kuwatungua Yanga uwanja wa Taifa (Sasa Uhuru).

Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 4-1, Madaraka alifunga bao hilo kwa shuti kali, lakini aliuseti mguuni kwake mpira kwa mkono, mwamuzi hakuona na akaweka kati, wakati huo Rais wa Yanga Tarimba Abbas Tarimba akawaamuru wachezaji wake watoke nje.

Lakini chama cha soka wakati FAT kikamfungia Rais huyo wa Yanga, ndivyo ilivyo Tanga jana, mwamuzi hakuona magoli yote ya Yanga kitendo cha kuwaadhibu si cha kiungwana, lakini yote yametokea kwa sababu ya TFF.

Wadau wa soka nchini walishangaa sana waliposikia TFF imezipeleka mechi za Nusu fainali kwenye viwanja vya mikoani ambavyo havina hadhi ya kuchezea mashindano hayo, Tanga hakuna usalama kama ambao ungechezwa uwanja mkuu wa Taifa.

Samahani sana ndugu zangu wa mkoa wa Tanga kwa kuwaambia uwanja wenu wa Mkwakwani ni uchochoroni, lakini hayo yote yamesababishwa na mechi ya jana ambapo mwamuzi maaidizi alishambuliwa na mashabiki wa Coastal.

Kama ingetokea mwamuzi wa pambano hilo kuaga dunia basi TFF ingekuwa lawamani kwakuwa ilishataadhalishwa mapema mechi hizo kupelekwa "vichochoroni" kwani mawe ya jana ni sawa na mechi kuchezwa uchochoroni.

Tuonane tena juma lijalo, napatikana kwa namba 0652626627

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA