ANAYEKUMBUKWA: ABDALLAH KIBADENI, MUUAJI WA MABAO MATATU PEKEE SIMBA NA YANGA
Na Ikram Khamees, DAR S SALAAM
HAKIKA kabisa miaka ya 70 gwiji la soka wakati huo alikuwa Abdallah Seif Athuman, Wangoni wakampachika jina la Kibadeni na wakamuongezea lingine la King Mputa.
Kibadeni alikuwa mfanisi wa soka uwanjanj, kwa wale waliobahatika kumuona akisakata kandanda hawana shaka naye, kwakweli alikuwa fundi wa mpira.
Ingawa historia zinaonyesha alikuwa klabu ya Simba na alitamba na klabu hiyo, lakini yeye mwenyewe aliweka bayana kuwa ilikuwa kidogo aichezee Yanga, anasema alianza kujiunga na Yanga lakini akakataliwa.
Kisa cha kukataliwa kwanza kilikuwa kimo chake kidogo lakini pili bangili, anadai yeye hupendelea kuvaa bangili mkononi hivyo Yanga walimtaka avue akakataa na ndipo alipoamua kuachana nao na kupelekwa Simba.
Alivuma na Simba pamoja na Taifa Stars kabla ya kujiunga na Majimaji ya Songea alikopachikwa jina la Kibadeni, alirejea Simba na kuendeleza makali yake.
Kibadeni ana rekodi yake moja ambayo bado inashindwa kuvunjwa, mshambuliaji huyo akiwa Simba mwaka 1977 alifanikiwa kuitungua Yanga mabao matatu mguuni kwake (Hat trick).
Katika mchezo huo wa ligi kuu bara, Simba iliifunga Yanga mabao 6-0 ambayo ni mengi kwani tangu mwaka huo si Simba wala Yanga hakuna timu iliyomfunga mwenzake mabao kama hayo na pia hakuna mchezaji yeyote wa Simba wala Yanga aliyetupia mabao matatu kwenye mchezo mmoja.