STARS WAJIFUA VIKALI D'JAMENA, MKWASSA AAHIDI USHINDI UGENINI
Na Elias John, D'jamena
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo kimejifua vikali katika uwanja wa Amnisports Idris Mahanat uliopo hapa D'jamena na kwa mara ya kwanza nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta aliwaongoza wenzake.
Stars itashuka dimbani jumatano ijayo kukabiliana na wenyeji wao Chad mchezo wa mchujo mataifa barani Afrika.
Kocha mkuu wa Stars Charles Boniface Mkwassa amewaahidi Watanzania kwamba atachomoza na ushindi katika mchezo huo ambao unatarajia kuwa mkali na wa kusisimua.
Mkwassa amedai anataka kiwashangaza Watanzania kwa kupata ushindi wa ugenini kama ilivyokuwa kwa vilabu vya Yanga na Azam ambavyo vyote vilishinda katika mechi zao za mashindano ya Afrika.
Nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji naye amewataka Watanzania kuwaombea dua ili waweze kufanya vizuri, Stars na Chad zinatarajia kurudiana mwishoni mwa wiki hii katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam