STAA WETU: BATAROKOTA, ANA VIPAJI VINGI VYA KUJIVUNIA, NDIYE ALIYEITENGENEZA BLOGU HII
Na Salum Fikiri Jr, MOROGORO
Nilisafiri hadi mjini Morogoro maeneo ya Kihonda ili nikutane na jamaa mmoja anayafahamika kwa jina la Paschal Linda ama waweza kumuita Batarokota.
Unaweza kujiuliza maswali mara mbili mbili hasa nilipotaja jina la Batarokota ambalo si geni masikioni na machoni kwenu, jina hili lilichomoza mwaka juzi kwenye tuzo za Kill Music Awards 2014 ambazo zilimwezesha msanii Diamond Platinumz kuzoa tuzo saba kwa mkupuo.
Batarokota alikuwemo katika tuzo hizo baada ya kuteuliwa kuingia kwenye kategoli, Batarokota alipata nafasi ya kuingia kwenye tuzo hizo na wimbo wake wa 'Kwejaga nyangisha' ambao ni wa asili na ameuimba kwa lugha ya Kisukuma.
Kwa bahati mbaya Batarokota hakupata tuzo ila aliweza kujitambulisha vema kwenye medani ya muziki kwani wasanii wengi tu hapa nchini wenye majina makubwa hawakuwahi kuingia kwenye tuzo hizo.
Awali Batarokota alikuwa akiimba hip hop na alibahatika kurekodi nyimbo nne ambazo zote ameziweka Youtube hivyo ukizihitaji unaweza kuzipata, wimbo wa 'Sauti ya haki' na 'Vichwa vya gola' ni moja kati ya nyimbo nzuri ambazo zinamweka katika orodha ya wasanii wanaofanya vizuri.
Batarokota anasema aliamua kuimba muziki wa asili baada ya kuombwa na baadhi ya mashabiki wake, "Waliniona nafaa kuimba muziki wa asili, hivyo nikaamua kuimba ili niwafurahishe, mimi ni msukuma mwenyeji wa Mwanza nikaamua kuimba Kisukuma", alisema Batarokota, baba wa watoto wawili Sarah na Linda.
Msanii huyo aliyezaliwa miaka 40 iliyopita jijini Mwanza, ameongeza kuwa muziki upo ndani ya damu yake, anasema alianza kuimba tangia anasoma shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu cha St Agustino baadaye Nairobi Kenya.
Aliwahi kushinda tuzo akiwa chuoni katika mashindano ya muziki, "Hapo ndipo nilipokutana na watu wangu wa Gola ambao nimefanya nao Collabo iitwayo "Vichwa vya Gola", anasema.
Aidha Batarokota anaelezea taaluma yake nyibgine aliyoisomea chuoni, anasema yeye ni mtaalamu wa kutengeneza Webbsite na tovuti na ndiye aliyeitengeneza tovuti ya Mambo Uwanjani aambayo leo hii imekuwa tovuti bora hapa nchini.
Amewataka Watanzania hasa wafanyabiashara kutosita kuonana naye ili awatengenee tovuti kwa ajili ya kutangaza biashara zao, msanii huyo tayari ameingia tena studio kutengeneza wimbo mwingine wa asili ambao anabashiri utakuwa mkali kuliko ule wa kwanza uliomwingiza tuzo za Kill.
AMSIKITIKIA CHID BENZI
Batarokota ameonyesha masikitiko yake kwa msanii wa hip hop Rashid Makwiro maarufu Chidi Benzi ambaye kwa sasa anasumbuliwa na maradhi yaliyotokana na matumizi ya dawa za kulevua, Batarokota anawaasa wanadamu wenzake kutomcheka Chidi Benzi wala kumdhihaki kwani tatizo alilonalo linaweza kumkuta mtu yeyote.
"Yaliyomkuta Chidi Benzi yanaweza kumtokea mtu yeyote yule kwani hata yeye hakupenda imtokee hivyo", alisema Batarokota ambaye kwa sasa anaishi Morogoro.
UNAFAHAMU KWAMBA NI MCHUNGAJI
Batarokota ana vipaji vingi, moja wapo ni hili la uchungaji, jamaa ni mchungaji lakini si mlokole, yeye ni mchungaji wa makanisa ya Kikatoliki na amekuwa akitoa maneno mema ya kumfurahisha mwenyezi mungu.
TUKUTANE TENA JUMA LIJALO