MAONI: SIMBA ITANUFAIKA NA VIPOLO VYA YANGA NA AZAM
Na Prince Hoza
Kwanza ningeanza kwa kuzipongeza timu za Yanga na Azam kwa ushindi wao walioupata katika michuano ya kimataifa na kuiwakilisha vema nchi yetu ya Tanzania.
Yanga iliifungasha virago APR ya Rwanda kwa kuifunga jumla ya mabao 3-2, Azam nayo imeitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3, sasa timu hizo zimetinga raundi ya pili.
Kwenye mada yangu ya leo naizungumzia klabu ya Simba yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi Kariakoo jijini Dar es Salaam, hivi karibuni uongozi wa Simba ulitishia kutoingiza timu uwanjani mpaka pale Yanga na Azam zitakapocheza mechi zake za ligi ili kusiwepo na vipolo.
Yanga na Azam wana vipolo vya mechi tatu dhidi ya Simba ambayo hadi sasa imecheza mechi 24 huku Yanga na Azam zimecheza mechi 21, Simba wametishia kugoma na wakiitaka TFF kuzipangia mechi Yanga na Azam ili zikamilishe vipolo vyao.
Yanga na Azam zimeshindwa kucheza mechi zake za ligi kwakuwa zibabanwa na ratiba ya michuano ya kimataifa, Yanga inawakilisha taifa ikishiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wakati Azam yenyewe inashiriki kombe la shirikisho barani Afrika.
Lakini Simba hawataki kusikia hilo, wanataka kuona Yanga na Azam zinacheza mechi zake ili mwisho wa ligi kusiwepo na suala la kupanga matokeo, malalamiko ya Simba mimi nayaunga mkono kwani kwa upande mwingine yanaibeba Simba.
Simba imekuwa ikipata matokeo mazuri katika mechi zake za ligi huku Yanga na Azam zikisaliwa na vipolo, vipolo vya Yanga na Azam vinaweza kuisaidia Simba kwani hadi sasa inaongoza ligi tena ikiwa na pointi 57 huku hao Yanga na Azam wanapointi 50.
Uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa ndiyo yanazigawa timu hizo mbili, Simba wanataka kugomea ligi na TFF imesema wataihsusha daraja iwapo itathubutu kufanya hivyo.
Simba inaweza kubebwa na vipolo vya Yanga na Azam kwani timu hizo zinaweza kukutana na changamoto ya ushindani kutoka kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo, kuna uwezekano mkubwa Yanga ikakutana na timu zinazopigania kubaki ligi kuu hivyo zikawapa ushindani ama kutokukubali kufungwa na kulazimisha sare ambayo itaisaidia sana Simba.
Pia Yanga inaweza kupoteza kwani hakuna timu ambayo haijawahi kufungwa, Simba ina mtaji mkubwa wa pointi wakati Yanga na Azam zina mtaji wa vipolo ambavyo vinaweza kuchacha.
Kama Wanasimba watakuwa makini na matokeo mazuri inayopata bila kuwaangalia Yanga na Azam inaweza kunufaika, lakini kama itachungulia wenzake basi inaweza kujikuta inaambulia patupu.
Kiukweli kabisa Watanzania tunapaswa kuwa kitu kimoja ili kuziunga mkono Yanga na Azam ambao ndio wawakilishi wetu pekee katika michuano ya kimataifa.
Endapo Yanga na Azam zitapewa muda wa kujiandaa basi zinaweza kufanya vizuri, Yanga itakutana na miamba ya Misri National Al Ahly wakati Azam itakutana na miamba ya Tunisia Esperance, Simba tumieni nafasi hii mnayoipata ya kutangulia kucheza kwani inaweza kuwanufaisha mwisho wa ligi.
Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa soka hapa nchini na anapatikana kwa namba 0652626627.