SAMATTA AWATOA HOFU WATANZANIA KUHUSU MLIPUKO WA MABOMU UBELGIJI
Na Elias John, D'jamena
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars Mbwana Ali Samatta amewatoa hofu ndugu zake na Watanzania kwa ujumla kuhusu milipuko ya mabomu iliyotokea mjini Brusseils Ubelgiji.
Samatta ambaye anachezea KRC Genk ya Ubelgiji hakuwepo kabisa nchini Ubelgiji wakati milipukp hiyo ilipotokea, milipuko hiyo ilitokea juzi jumanne wakati mchezaji huyo tayari alikuwa mjini D'jamena na timu ya taifa.
Akizungumza na Mambo Uwanjani mara baada ya kumalizika mchezo kati ya Tanzania na Chad, ambapo Tanzania ilishinda 1-0 huku mfungaji wa bao pekee la Tanzania akiwa ni yeye, Samatta amesema yeye hakuwepo kabisa hivyo ni ngumu kuandika habari kuwa alinusurika.
Gazeti moja la michezo nchini Tanzania (Jina tunalo) liliandika Mbwana Samatta alinusurika katika milipuko hiyo ya mabomu jambo ambalo lilizua utata kwa ndugu zake, jamaa na marafiki.
"Sikuwepo kabisa Ubelgiji, niko hapa D'jamena tangu jumatatu na milipuko imetokea jumanne ni jambo la kichekesho kusema nilinusurika", alisema nahodha huyo.