NANI KAKWAMBIA KIPORO KINACHACHA KWA YANGA, YAIKANDIKA 2-1 NDANDA, YATINGA NUSU FAINALI
Na Salum Fikiri Jr, DAR ES SALAAM
Mabingwa wa soka nchini Yanga Sc jioni ya leo imeichapa timu ya Ndanda Fc ya Mtwara mabao 2-1 katika uwanja wa Taifa Dar ea Salaam mchezo wa robo fainali kombe la Azam Sports Federation Cup maarufu FA Cup.
Yanga wakicheza kwa taadhali kubwa walijipatia bao la kuongoza kunako dakika ya 35 kipindi cha kwanza likifungwa na mshambuliaji wake Poul Nonga ambaye leo amecheza vizuri.
Hadi mapumzikp Yanga walikuwa mbele kwa goli hilo, kipindi cha pili timu zote zilirudi uwanjani na Ndanda walionekana kucharuka wakitaka kusawazisha bao hilo, iliwachukua muda mfupi baadaye Kiggi Makassy winga wa zamani wa Yanga na Simba aliisawazishia Ndanda na kuwa moja kwa moja.
Poul Nonga kwa mara nyingine alimpa pasi nzuri Simon Msuva ambaye alikuwa anaingia na mpira langoni mwa Ndanda kabla ya beki Poul Ngalema kumkwatua na mwamuzi kuipa penalti Yanga.
Mwamuzi huyo pia alimpa kadi nyekundu mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Simba na kuwafanya Ndanda kucheza pungufu, Kelvin Yondani aliipatia Yanga bao la pili na la ushindi kwa mkwaju wa penalti.
Yanga sasa imeingia nusu fainali ya kombe la FA na inaungana na Mwadui Fc ya Shinyanga iliyowaduwaza ndugu zao wa Geita Gold ya Geita kwa mabao 3-0