MICHANO: DAZ BABA NAYE ANAHITAJI MSAADA KAMA CHID BENZI
Na Mkola Man, TANGA
YAP...yap...yap...Michano leo inamchana Daz Baba mwanaharakati aliyetumbukia kwenye shimo la madawa ya kulevya, kiukweli amepoteza mwelekeo ingawa kazi ni kazi ila inasikitisha pale anapoendesha maisha yake kwakupiga debe kwenye vituo vya daladala.
Huyu jamaa alikuwa kiongozi wa kundi kubwa na maarufu la muziki wa kizazi kipya la Daz Nundaz lenye maskani yake Sinza Dar es Salaam, kundi hilo lilijumuhisha wasanii watano akiwemo yeye.
Ila kwa sasa kundi hilo halipo tena yaani kwa maana nyingine limekufa, Daz Nundaz lilijipatia unaarufu mkubwa hasa kwa kuimba nyimbo za huzuni kama Kamanda, Maji ya shingo, Barua na nyinginezo nyingi.
Aidha Daz Baba binafsi amepata kutamba na nyimbo zake kama Elimu dunia, Umbo namba 8, Wife, Nipe tano na nyingine, kwa sasa jamaa anahitaji msaada wa kutupiwa kamba ili aishike na atoke kwenye shimo la madawa ya kulevya.
Kama mmeweza kumpa kamba Chid Benz basi kamba hiyo mpeni na Daz Baba kiongozi wa zamani wa kundi la Daz Nundaz lililojumuhisha vichwa kama Ferooz Mrisho, Sajo, Larhumba, Critic na Daz mwenyewe.
Hata hivyo inaonyesha tabia ya kuiga na kukata tamaa ndio chanzo cha matumizi ya madawa ya kulevya, Michano inamshauri Daz Baba anapochoma kuni asishangae majivu.
Tukutane Wiki ijayo kwenye Michano inayojenga na si kubomoa inayotayarishwa na Rapa Mkola Man mwenye chimbo lake Hale jijini Tanga, Ciao