MAONI: KIMAHESABU YANGA NA AZAM ZIMESHATOLEWA CAF

Na Prince Hoza, DAR ES SALAAM

KWANZA naanza na hii ya kutofanyika kwa mchezo wa kufuzu fainali za mataifa Afrika kati ya Tanzania na Chad ambao ulikuwa uchezwe leo Machi 28 uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ina maana CAF itaifungia Chad na kuitoza faini, vilevile matokeo yake yote kufutwa, hivyo Tanzania itabakiwa na pointi yake moja, huku Misri ikiendelea kuwa kinara na pointi nne.

Itakuwa ngumu tena Tanzania kufuzu kwenye kundi G kwani limesaliwa na timu tatu na litakosa nafasi ya kutoa 'Best Rooser' na kuinyima nafasi nchi yetu kufuzu kwa mara ya pili fainali hizo za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Gabon.

WAWAKILISHI WENGINE WA TANZANIA NAO SHAKANI.

Tanzania ina wawakilishi wengine wawili katika mashindano ya vilabu barani Afrika, wawakilishi hao ni Yanga Sc na Azam Fc.

Yanga Sc inashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wakati Azam Fc inashiriki michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, timu zote hizo zimetinga raundi ya pili na zote zinakabiliwa na mechi ngumu mwanzoni mwa mwezi ujao.

Yanga itaanza na miamba ya Kaskazini, Al Ahly (National) mchezo wa kwanza ukianzia Dar es Salaam na marudiano yakifanyika Cairo, Yanga na Al Ahly watacheza April 9 na marudiano April 19 au 20.

Wakati Azam Fc wataikaribisha Esperance ya Tunisia mchezo wa kwanza ukifanyika Azam Complex na marudiano jijini Tunis, mechi ya Azam na Esperance zitachezwa April 10 na marudiano April 21.

Lakini nina wasiwasi na timu hizo za Tanzania, kwanza zinakutana na miamba ya Afrika, Al Ahly na Esperance ni washindani wa kweli katika michuano yote ya Afrika na zimekuwa zikipambana haswa kila michuano hiyo inapofanyika, Al Ahly na Esperance lazima zitafika hatua ya makundi.

Timu za Tanzania mara yake ya mwisho kucheza hatua ya makundi ni mwaka 2003 wakati Simba Sc ilipofanya hivyo.

Lakini ufinyu wa ratiba ya ligi kuu ndio inayopelekea hofu ya kutolewa kwa wawakilishi hao wote wawili, Yanga itapata siku mbili tu kujiandaa na Al Ahly kwani inabanwa na ratiba ya ligi kuu bara na kombe la FA.

Yanga na Azam zote zimepangiwa mechi nne za mashindano ya ndani, tatu za ligi kuu na moja kombe la FA, mechi hizo wataanza kuzicheza mwishoni nwa wiki hii.

Yanga wamebanwa na ratiba hivyo hawatapata muda wa kujiandaa dhidi ya Al Ahly ambao wao watacheza mchezo mmoja tu wa ligi ya kwao Misri kabla kuivaa Yanga, hakuna asiyetambua uwezo wa Waarabu hao wa kaskazini, Azam nao wamebanwa na ufinyu wa ratiba yao ya ligi.

Ili timu hizo mbili zijiandae angalau TFF na Bodi ya ligi zingeangalia utaifa zaidi na kuzipa muda wa kujiandaa na mapambano hayo, kama Watanzania tunataka mafanikio katika michuano ya kimataifa tuondoe ushabiki na kuziunga mkono Yanga na Azam, ushabiki utaifanya Tanzania kutokuwa na mwakikishi wowote katika mashindano ya CAF isitoshe timu yetu ya taifa imeshapotezewa mwelekeo na Chad.

Tukutane wiki ijayo, nawatakia kila la kheri Pasaka njema.

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa soka hapa nchini na anapatikana kwa namba 0652626627.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA