MAONI: SIMBA IACHE VISINGIZIO, IKUBALI ILIZIDIWA MBINU NA YANGA

Na Prince Hoza

Simba Sc juzi jumamosi ilikubali kichapo cha mabao 2-0 toka kwa mahasimu wao Yanga Sc katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam mchezo wa ligi kuu bara.

Jumla Simba imefungwa na Yanga mara mbili ndani ya msimu huu, kuelekea katika mchezo huo, timu zote zilijiandaa vema.

Simba ndiyo iliyokuwa katika morali ya hali ya juu kwani ilikuwa ikifanya vizuri katika mechi, ushindi mfululizo ilioupata dhidi ya Kagera Sugar 1-0 na Stand United 2-1 zote ikishinda ugenini uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ziliwapa hamasa kubwa wapenzi na mashabiki wake.

Ushindi huo uliipeleka kileleni Simba na kuwafanya watambe, tofauti na mahasimu zao Yanga ambao waliambulia pointi moja katika mechi zake mbili za ugenini.

Yanga ilifungwa mabao 2-0 na Coastal Union uwanja wa Mkwakwani Tanga, kisha kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Prisons uwanja wa Sokoine Mbeya, matokeo hayo yaliwasononesha sana mashabiki wa timu hiyo na walianzabkuikatia tamaa timu yao.

Licha kwamba Yanga ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, lakini ushindi huo haukupokelewa kwa furaha na Wanayanga.

Wanayanga wanafahamu uwezo wa wapinzani wao Cercle kuwa ni wa chini mno hivyo mawazo yao waliyaelekeza kwa Simba, pia hawakuupokea kwa furaha ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu.

Hivyo matumaini ya kuifunga Simba yalikuwa madogo, Yanga waliweka kambi yao kisiwani Pemba na hawakutaka kuzungumza na chombo chochote cha habari kuelekea mchezo wake  na Simba.

Simba nao walisikika wakitamba kwenye vyombo vya habari na mara kwa mara viongozi wake kuanzia msemaji wa timu hiyo Hajji Manara na nwenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hanspoppe walisikika wakitamba na kudai wataifunga Yanga.

Hakuna shabiki wa soka asiyejua makali ya kikosi cha Simba, Hamisi Kiiza "Diego" na Ibrahim Ajibu wamekuwa katika kiwango cha juu na kuzidi kuwatisha mabeki wa Yanga.

Simba iliweka kambi yake mjini Morogoro na kocha wake Jackson Mayanja alikuwa akinukuliwa kwamba vijana wake wako tayari kuimaliza Yanga, lakini viongozi wa Yanga walikaa kimya na hawakutoa ushirikiano wowote.

Lakini ilipotimia siku ya mpambano wenyewe, Februali 20 Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0, goli la kwanza la Yanga lilipatikana kipindi cha kwanza likifungwa na Donald Ngoma na la pili lilipatikana kipindi cha pili likifungwa na Amissi Tambwe.

Mwamuzi wa kati Jonnesia Rukyaa alimtoa mapema beki wa Simba Abdi Banda baada ya kuonyeshwa kadi mbili za manjano, goli la kwanza la Yanga lilitokana na juhudi binafsi za mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma ambaye aliutokea mpira uliokuwa ukirudishwa kwa kipa na Hassan Kessy.

Pia goli la pili lilifungwa na Tambwe lakini zilikuwa juhudi zake binafsi kwani ilipigwa krosi na Geofrey Mwashiuya na kumkuta Tambwe mguuni kwake na kuuweka kimiani.

Tambwe alikaa na Juuko Murushid lakini mbinu zake ndizo zilizopelekea kufunga bao hilo, baada ya mpira kumalizika, viongozi wa Simba pamoja na mashabiki wake walisikika wakimlaumu mwamuzi wa mchezo huo wakidai ndiye aliyesababisha timu yao kufungwa na Yanga.

Simba wanadai timu yao imefungwa kwa sababu Abdi Banda alipewa kadi nyekundu mapema, kwangu hizo ni sababu za kitoto mno, Simba imewahi kuifunga Yanga mara kadhaa huku ikiwa pungufu baada ya mchezaji wake kupewa kadi nyekundu.

Ilishatokea sana kwa Haruna Moshi "Boban" na Victor Costa, sikuwahi kusikia akilalamikiwa mwamuzi baada ya kumalizika mchezo huo, iwejebtena safari hii mwamuzi anaoekana tatizo.

Hizo ni sababu za kitoto, mkubali tu matokeo kwani dhahili Yanga iliwazidi mbinu, mfumo walioutumia Yanga ulitosha kuwapa ushindi wa mabao 2-0, sitaki nielezee kiundani ila Simba mjipange na mkubali matokeo.

Tuonane tena wiki ijayo Inshallah

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA