MAONI: KUNA SIKU BONDIA ATAKAYETANGAZWA MSHINDI ATAPELEKWA NA AMBULANCE MUHIMBILI
Na Prince Hoza
Kwanza nianze kwa kutoa salamu zangu za pongezi kwa bondia Fransis Cheka hasa baada ya kutwaa ubingwa wa WBF juzi usiku katika ukumbi wa Leaders Club.
Ushindi wa Cheka ni furaha kwa Watanzania kwani alikuwa akipeperusha bendera ya nchi, lakini ushindi wake umetawaliwa na hujuma za hapa na pale kwani sikuona ngumi za ufundi.
Cheka ni Mtanzania mwenzangu lakini sioni umuhimu wowote kusifu pale ninapoona kuna makosa ya kiufundi.
Bondia aliyepambana na Cheka alionekana kuimarika zaidi huku akirusha makonde yenye nguvu yaliyokuwa yakimtetemesha Cheka na kuna wakati alikuwa akianguka.
Licha kwamba alionyesha ushujaa mkubwa kwa kutokubali kupigwa kwa Nock Out lakini alielemewa muda wote na kumfanya mpinzani wake aendelee kumkalia karibu.
Cheka alikuwa akipokea masumbwi ya usoni lakini Cheka alishindwa kundunda mpinzani wake usoni na ngumi zake nyingi ziliishia mikononi kwa mzungu huyo raia wa Serbia.
Mwamuzi wa mchezo huo alimtangaza Fransis Cheka mshindi wa pambano hilo jambo ambalo lilizua utata kwa Watanzania waliojitokeza kushuhudia pambano hilo.
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, ndivyo unavyoweza kutamka, sina shaka na ushindi wa Cheka ila hofu yangu ni kwamba kuna siku bondia atakayetangazwa kushinda kwa pointi anaweza akajikuta anatangazwa mshindi kwenye gari la kubebea wagonjwa Ambulance.
Hii ina maana kwamba mshindi anayetangazwa na majaji anakuwa majeruhi zaidi kuliko yule aliyepigwa, Cheka alitangazwa mshindi akiwa amepigwa ngumi nyingi za usoni na mpinzani wake kiasi kwamba Mserbia huyo alidai Cheka amebebwa.
TUONANE WIKI IJAYO