ETOILE DU SAHEL YAILIPA SIMBA MILIONI 600 ZA OKWI

KLABU ya Etoile du Sahel ya Tunisia imesema kwamba imekwishaweka fedha benki kwa ajili ya kuilipa Simba SC dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.

Mwenyekiti ya Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekutana kwa mazungumzo na Katibu wa Etoile, Adel mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) leo na amehakikishiwa kupata fedha zao wakati wowote.

"Baada ya kumaliza suala la Mazembe na samatta, leo nimekutana na katibu wa Etoile, Adel ambaye ameniambia jumatatu waliweka fedha benki kwa ajili ya kutulipa, sasa wajkati wowote mzigo utaingia dar es Salaam,"amesema Poppe juu ya fedha hizo, ambazo ni mauzi ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013.

Etoile, mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika wapo Lubumbashi kwa ajili ya mchezo wa kuwania taji la Super Cup ya CAF dhidi ya wenyeji, TP Mazembe ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika kesho Uwanja wa Mazembe mjini humo.
Hans Poppe (kulia) akizungumza na Katibu wa Etoile, Adel leo mjini Lubumbashi

Awali, Etoile walikuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.


Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu.
Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.

Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa.

Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote.

Hans Poppe alikwenda Lubumbashi,kuchukua mgawo wa Simba SC wa Euro 160,000 katika klabu ya TP Mazembe kutokana na mauzo ya mshambuliaji Mbwana Ally Samatta.

Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 kwa dau la Sh. Milioni 100,000 akitokea Simba SC na Januari mwaka huu amejiunga na klabu ya Koninklijke Racing Club Genk ya Ubelgiji kwa Mkataba wa miaka minne na nusu.

Mambo Uwanjani inafahamu Samatta ameuzwa Genk kwa dau la Euro 800,000 Genk kutoka Mazembe ambayo inalazimika kuipa Simba SC asilimia 20 ya pato hilo kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Samatta aliyezaliwa Desemba 23, mwaka 1992, ameondoka Mazembe baada ya kushinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, ubingwa wa Ligi Kuu ya DRC mara nne na Super Cup ya DRC mara mbili.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA