#MAONI: TFF IMEHODHI LIGI KWA AZAM
Na Prince Hoza
KITENDO kilichofanywa na shirikisho la kandanda nchini TFF kuiruhusu Azam Fc kwenda Zambia kucheza mechi za kirafiki na kuikacha ligi kiu ya Vodacom Tanzania bata huku ikisababisha kupangua ratiba ya ligi hiyo si cha kuzoeleka hata siku moja.
TFF imefanya kosa kubwa ambalo linaanza kuharibu sifa ya shirikisho hilo pamoja na Bodi yake ya ligi TPLB, Licha kwamba raisi wa shirikisho hilo Jamal Malinzi kuomba radhi lakini bado ni sawa na kazi bure, kwani kosa limeshafanyika.
Bora ruhusa hiyo ingepewa Mwadui Fc au Kagera Sugar sidhani kama wadau wa soka wangelalamika sana, huenda wangelisifu shirikisho hilo kwani timu hizo hazipo kwenye mbio za ubingwa, kitendo cha kuiruhusu Azam Fc kinaonekana kama cha kuipendelea.
Tunafahamu kwamba Azam Fc ni timu inayomilikiwa na bilionea Said Salim Bakhressa ambaye pia ndiye mmiliki wa Azam Tv yeye na familia yake.
Azam Tv ni wadhamini wenza wa ligi kuu bara hivyo ina nguvu ndani ya shirikisho hilo, matajiri hao pia wanadhamini michuano ya kombe la FA.
Azam Fc itakosa mechi mbili za ligi ambazo ilikuwa icheze na Prisons jumamosi iliyopita na Stand United jumatano ijayo, mechi hizo zilipaswa zichezwe pamoja na nyingine ili kusitokee suala la kupanga matokeo.
Azam Fc ipo kwenye mbio za kuwania ubingwa wa bara ikiwa katika nafasi ya pili na pointi zake 39 huku vinara wa ligi hiyo Yanga nao wakiwa na pointi kama hizo 39.
Simba wanakamata nafasi ya tatu na pointi zao 36, kitendo cha Azam kutimkia Zambia kunapelekea kupangwa kwa matokeo kwani imeziacha Yanga na Simba peke yao.
Tayari Yanga imecheza mchezo wake wa 16 na Coastal Union na ikapoteza kwa kifungwa mabao 2-0 katika uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam wameyapata matokeo hayo ya kufungwa kwa Yanga wakiwa mjini Ndola Zambia wanakoshiriki michuano isiyo rasmi.
Kwa vyovyote Azam imeshapata faida kwani mpinzani wake mkuu kwenye mbio hizo Yanga imeshateleza, Azam inahitaji pointi moja tu kuipoka Yanga uongozi.
Madudu ya TFF yanazidi kuendelea kwani kuiruhusu Azam peke yake kwenda kujiandaa na michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika ni dhahili kama inaiandaa Azam peke yao wakati Tanzania bara itawakilishwa na timu mbili ikiwemo Yanga.
Yanga itaiwakilisha bara katika michuano mikubwa kuliko yote kwa upande wa vilabu barani Afrika ambayo ni ligi ya mabingwa, hivyo TFF ilipaswa nayo kuipa Yanga muda wa maandalizi kama ilivyofanya kwa Azam.
Yanga ilipata mwaliko nchini Afrika Kusini lakini TFF iliwakatalia, hii inaonyesha kwamba shirikisho hilo limehodhi ligi kuu bara kwa Azam.
TUONANE TENA JUMATATU IJAYO
Call 0652626627