BEKI AFRICAN SPORTS ATUA SIMBA, MAJWEGA NAYE KIMEELEWEKA

Dirisha dogo la usajili Ligi Kuu Bara limefikia patamu, huku Simba, Yanga na Azam FC zikionekana kuwa kivutio kipindi hiki.

Wakati Yanga bado ikielekeza nguvu za usajili kumnasa mshambuliaji wa Stand United, Elius Maguli, watani wao wa jadi Simba wamemalizana na mlinzi, Novat Lufungo kutoka African Sports ya Tanga.

Wakati Wekundu hao wa Msimbazi wakimalizana na  Lufungo, pia hatua za mwisho kuipata saini ya winga wa Azam FC, Mganda FC Mganda, Brian Majwega.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi, zimethibisha usajili wa Lufungo aliyelamba Sh. milioni 10 ili kuvaa jezi nyeupe na nyekundu.


Mazungumzo ya Simba na mchezaji huyo yalikamilika Jumatatu usiku na tayari mchezaji huyo baada ya kumwaga wimo amekwenda kuungana na wenzake waliopiga kambi jijini Zanzibar.

Simba iko Zanzibar kujiandaa na mchezo Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC utakaochezwa Desemba 12 kwenye Uwanja wa Taifa.

Lufungo, nyota wa zamani Mgambo JKT, amesaini mkataba wa miaka miwili.

“Tumemfuatilia kwa muda mrefu, nashuruku tumemalizana naye salama na ameshakwenda kujiunga na wenzake Zanzibar,” alidokeza mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti kwa kuwa siyo msemaji.
“Huyu ni mchezaji mzuri, anaweza kucheza namba  4, 5 na 6,” aliongeza mtoa habari huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alithibitisha usajili wa mchezaji huyo. Makamu Mwenyekiti wa African Sports, Abdul Bosnia aliliambia gazeti hili kuwa Simba wamekamilisha taratibu zote za kumsajili beki huyo.

“Hatuna shida na Simba, wamekamilisha taratibu zote za usajili. Mambo mengine ni kati ya Simba na mchezaji mwenyewe,” alisema Bosnia.

Katika hatua nyingine, Manara alisema kuwa Majwega ambaye alikuwa akijifua na Simba, anatarajia kurejea nchini wakati wowote akitokea  Uganda.

Endapo Simba itafanikiwa kumsajili Majwega, itafikisha wachezaji wa kimataifa sita ambao wengine ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid kutoka Uganda, Justice Majabvi (Zimbabwe), Emery Nimubona (Burundi) na Vincent Angban wa Ivory Coast.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA