YANGA KUWAALIKA HEARTS OF OAK YA GHANA KUCHEZA KIRAFIKI

Katika kudhihirisha tambo za msemaji wao, Jerry Muro kwamba 'wao ni wa kimataifa', Yanga wamewaalika mabingwa wa Ligi Kuu ya Ghana, Hearts of Oak, kuja nchini kwa ajili ya mechi ya kirafiki.

Tangu aingie madarakani Januari, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga (Muro) amekuwa akitamba kuwa klabu hiyo ya Jangwani ni ya kimataifa.

Ili kufanya vyema katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani, Yanga wameanza kusaka mechi za kimataifa za kirafiki, safari hii wakikimbilia Ghana alikokuwa anafanyia kazi kocha mkuu wao, Hans van der Pluijm.

Jonas Tiboroha, Katibu Mkuu wa Yanga, aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa tayari walishapeleka barua ya maombi katika klabu hiyo kongwe inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana na wanaamini wataukubali mwaliko wao.

Tiboroha alisema programu ya benchi la ufundi, imeelekeza timu yao ipate mechi mbili za kirafiki kabla ya ligi haijaendelea na wanaamini watapata mechi hizo ili kukiimarisha zaidi kikosi chao.


"Tunasubiri majibu, ila tunaamini watakubali maombi yetu, hasa kupitia kocha wetu Pluijm (Hans) ambaye aliwahi kufanya kazi Ghana na kufahamiana na viongozi mbalimbali," alisema Tiboroha.

Aliongeza kuwa mshambuliaji wao wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma alirejea nchini juzi wakati kiungo wao Mbrazi Andrey Coutihno naye alitarajiwa kutua jijini jana usiku.

"Kuanzia kesho (leo) Jumatatu mazoezi yetu yatachanganya kwa sababu wachezaji wetu wa kimataifa waliokuwa nje ya nchi wataanza kujinoa na wenzao baada ya kuwa nje ya timu kwa sababu mbalimbali," alisema.

Kiongozi huyo alisema watahakikisha wanatekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na kocha wao ili waiimarishe timu na kufanya vizuri katika mashindano yote ya kimataifa watakayochuana mwakani.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA