WACAMEROON WATUA MSIMBAZI
Wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Cameroon, wamewasili nchini juzi usiku kwa ajili ya kufanya majaribio na timu ya Simba ya Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana kiongozi mmoja wa Simba (jina tunalihifadhi) alisema kuwa wachezaji hao wanacheza nafasi ya ushambuliaji.
Kiongozi huyo alisema wachezaji hao wameletwa na wakala mmoja aliyegharamia safari za wachezaji hao na mahitaji mengine kwa siku zote watakazokuwa nchini kufanya majaribio.
“Wakala aliyemleta Doumbie Ernest, ndiye jana (juzi) usiku, amewapokea wachezaji hao wawili kwa ajili ya kufanya majaribio Simba,” kilisema chanzo chetu.
Doumbie aliyewahi kuichezea Leopard FC inayoshiriki Ligi daraja la pili nchini Cameroon, mwishoni mwa wiki alionekana kwenye mazoezi ya Simba yanayofanyika kwenye fukwe ya Coco pamoja na winga Mganda, Brian Majwega.
Afisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema jana kuwa bado wachezaji hao wako mikononi mwa wakala aliyewaleta na Simba haijafanya nao mazungumzo yoyote.
“Ni kweli wachezaji wamefika, ila hawajaletwa na Simba, kuna wakala ndio kawaleta kwa ajili ya kujaribiwa, gharama ni zote za kuwaleta klabu haijahusika,” Manara alisema.
Aliongeza kwamba kikosi cha timu hiyo leo kinatarajia kuendelea na mazoezi kujiandaa na mechi yake ya raundi ya 10 dhidi ya vinara wa ligi, Azam FC itakayofanyika Desemba 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.