MAKALA: UNAMKUBUKA LUCAS NKONDOLA? MCHEZAJI ALIYEWEZA KUCHEZA NAFASI NYINGI UWANJANI
Kilimanjaro Stars ilikuwa timu ya kwanza kujikatia tiketi ya kucheza robo fainali baada ya kushinda mechi zake mbili mfululizo za mwanzo, ikumbukwe michuano ya Chalenji ndiyo michuano mikubwa kuliko yote katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati.
Lakini pia ndiyo michuano mikongwe kuliko yote barani Afrika, michuano ya Chalenji inasadikika ilianzishwa mwaka 1924, na kwa mara ya kwanza Tanzania bara baada ya uhuru ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 1974 ikiwa na kikosi bora kabisa ambacho kinatajwa hakijawahi kutokea.
Kikosi hicho golini alisimama Omari Mahadhi Bin Jabir (sasa marehemu), beki wa kulia alicheza Zaharani Makame, wakati beki wa kushoto alicheza Mohamed Chuma (sasa marehemu), namba nne alicheza Salim Amir wakati sentahafu alisimama Mohamed Bakari 'Tall', namba sita alisimama Jellah Mtagwa, namba saba alicheza Godfrey Nguruko ambaye baadaye kipindi cha pili alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Shiwa Lyambiko.
Namba nane alicheza Sunday Manara 'Computer', wakati sentafowadi alisimama Mwinda Ramadhan, namba kumi alicheza Gibson Sembuli (sasa marehemu) na kumi na moja alicheza winga ya maajabu Lucas Nkondola.
Kati ya wachezaji wachache waliokuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi wawapo uwanjani ni huyu Lucas Nkondola, kwani alimudu kucheza vyema nafasi ya ulinzi wa kushoto namba tatu, kiungo namba sita na nane pia nafasi ya ushambuliaji wa kushoto namba kumi na moja.
Pamoja na kutamba akiwa na timu ya taifa katika miaka hiyo ya 1970, pia kutokana na umahiri wake wa kusakata soka ameweza kuzichezea timu za Pamba FC ya Mwanza, Sungura FC ya Tabora, Simba SC ya Dar es Salaam, na katika mashindano ya kombe la Taifa Cup, Nkondola aliwahi kuzichezea timu za mikoa mbalimbali.
Aliwahi kuichezea timu ya mkoa ya Mwanza, (Mwanza Heroes), timu ya mkoa wa Shinyanga (Ingenisabo), timu ya mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima) na pia kuichezea timu ya taifa ya vijana.
Katika mchezo wa fainali ya mashindano ya Chalenji mwaka 1974, Nkondola ndiye aliyefunga bao pekee kwa upande wa timu ya taifa ya Tanzania bara wakati huo ikijulikana Taifa Stars (sasa Kili Stars), katika dakika ya 25 ya kipindi cha kwanza, kabla ya Uganda Cranes kusawazisha bao hilo katika dakika ya 85.
Pia katika upigaji wa penalti, Nkondola alifunga penalti moja kati ya tano zilizopatikana kwa upande wa Stars siku hiyo, kwa hivi sasa Nkondola anaishi Magomeni jijini Dar es Salaam akijishughurisha na kazi zake binafsi.
Nkondola pia ana mengi ya kukumbukwa alipokuwa na klabu ya Simba ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa, mchezaji huyo hatoweza kusahaulika kutokana na uwezo wake mkubwa aliowahi kuuonyesha