MAKALA: SIMBA ILIPOTEA MABOYA KWA ANGBAN, IMRUDISHE TU IVO MAPUNDA
YALIKUWA maamuzi ya kukurupuka na yasiyokuwa ya kitaaluma kumtema kipa mahiri Ivo Philip Mapunda kwa kisingizio kisicho na maana yoyote, ilikuwa rahisi Simba kumpa mkataba kipa Vincent Angban raia wa Ivory Coast, pia ilikuwa ngumu kumpa mkataba mpya Ivo Mapunda.
Bado kikosi cha Simba kinamuhitaji kipa kama Ivo Mapunda, Simba inaonekana ina mapungufu langoni kwake, mechi zote ilizocheza za ligi kuu bara, amedakaPeter Manyika Jr.
Manyika Ndiye yule aliyepigiwa hesabu za kutolewa kwa mkopo, ndiye yule aliyepotezewa na mashabiki na baadhi ya viongozi kutokana na dharau zake alizozionyesha msimu uliopita, lakini Muingereza Dylan Kerr aliamua kumtumia katika mechi tano za mwanzo ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara na kuonyesha kiwango.
KWANINI PETER MANYIKA JR
Dylan Kerr aliamua kumtumia Peter Manyika Jr kwenye mechi zake za mwanzo mznguko wa kwanza ligi kuu bara baada ya kumuona katika michezo ya kirafiki iliyofanyika Zanzibar.
Simba iliweka kambi yake Visiwani Zanzibar hivyo ilicheza mechi kadhaa za kirafiki, lakini kocha huyo hakuwa na malengo ya kumtumia Manyika Jr hasa akiamini mlinda mlango Vincent Angban ndiye chaguo la kwanza.
Angban alisajiliwa na Simba baada ya kucheza vizuri kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa na SC Villa ya Uganda uliofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba ikishinda 1-0.
Mchezo ulikuwa wa kuhitimisha sherehe za klabu hiyo zinazofanyika Agosti 8 kila mwaka maarufu 'Simba Day', baada ya kipa huyo kucheza vizuri alipewa mkataba wa miaka miwili na kuwa kipa wa kwanza wa timu hiyo badala ya Ivo Mapunda ambaye baadaye aliachwa.
Simba iliamua kumtema Mapunda kutokana na proglamu ya kocha ambaye alitaka awe na kipa mmoja mwenye uwezo mkubwa na wengine vijana, tayari Simba ilikuwa na makipa vijana watatu ambao ni Peter Manyika Jr, David Kissu na Dennis Richard.
CHANZO CHA KUKAA BENCHI ANGBAN HIKI HAPA
Kuachwa kwa Mapunda kulizua sintofahamu nyingi hasa ikiaminika kuwa kipa huyo alikuwa tegemeo kwenye kikosi hicho msimu uliopita, Kerr alimtumia Angban katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU uliofanyika uwanja wa Amaan Zanzibar.
Simba ilifungwa mabao 2-0, lakini magoli yote ya JKU ni uzembe wa kipa Angban ambaye aliwahi kufanya majaribio Chlesea ya England, Kerr aliamua kumpumzisha na kumwingiza Peter Manyika Jr ambaye alicheza vizuri bila kuruhusu goli.
Muingereza huyo aliyewahi kuichezea Sheffeild Wednesday ya England aliendelea kumtumia Manyika katika mechi zote zilizosalia huko visiwani Zanzibar, Manyika hakuruhusu bao hivyo aliridhishwa moja kwa moja na kiwango chake.
Manyika alianza kukaa golini katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu bara dhidi ya African Sports uwanja wa Mkwakwani Tanga, Simba ikishinda 1-0, Manyika alicheza vizuri na kuendelea kumfurahisha Muingereza huyo, pia alicheza vizuri kwenye mchezo mwingine dhidi ya Mgambo JKT, Simba ikishinda 2-0.
Manyika aliruhusu goli lake la kwanza kufungwa msimu huu, Simba ikiifunga Kagera Sugar 3-1 uwanja wa Taifa Dar es Salaam, akaendelea kukaa golini na kuzidi kumweka benchi kipa wa kimataifa Vincent Angban kwenye mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga uliofanyika uwanja huo huo wa Taifa.
Katika mchezo huo Simba ilifungwa mabao 2-0 na kuwaacha vichwa chini mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, pia Manyika aliendelea kukaa golini kwenyemchezo mwingine wa tano dhidi ya Stand United ya Shinyanga, Simba ikishinda 1-0 uwanja wa Taifa.
UMUHIMU WA IVO MAPUNDA
Ivo Mapunda (pichani) akiwa anawasalimia wachezaji wa Yanga wakati timu hizo zilipokutana mwaka juzi
Bado kipa Ivo Mapunda mwenye umri wa miaka 31 ni muhimu kwenye kikosi cha Simba, Mapunda alikuwa kipa wa kwanza katika kikosi hicho msimu uliopita huku Peter Manyika Jr akisota benchi, Mapunda anastahili kurejeshwa Simba kutokana na msaada wake mkubwa aliokuwa akiutoa msimu uliopita.
Haiwezekani kipa aliyesajiliwa kwa mamilioni ya shilingi tena wa kimataifa anaanzia benchi mbele ya chipukizi Manyika Jr, si kwamba nabeza uwezo wake au Manyika, naomba tu Simba imrudishe haraka Mapunda wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Siku moja niliwahi kuzungumza naye akaniambia kuachwa kwake kunaweza kuwanufaisha Yanga, na ni kweli baada ya kuachwa kwake, Wanayanga walifurahia, na walijitamba kuwa lazima waifunge Simba wakikutana, hilo limetokea hivi karibuni Simba ikilala 2-0 uwanja wa Taifa.
Yanga walionekana kufurahia, wanajua umuhimu wake katika kikosi hicho cha Simba, akikaa golini washambuliaji wa Yanga wanachachawa wenyewe, wanapaisha tu mashuti yao, wanaogopa taulo lake linalotanda golini, endapo Mapunda atarejeshwa Yanga watakuwa wapole.
Mapunda bado ni muhimu sana katika kikosi hicho kama ilivyo kwa Emmanuel Okwi ambaye pengo lake bado halijazibika