Lowassa aiteka Kusini
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akitangaza
kuahirishwa mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa chama hicho
anayeungwa mkono na vyama vya Ukawa Edward Lowassa kutokana na hitilafu
ya mitambo ya vipaza sauti.
Baadhi ya wananchi walikesha kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Tunduma, wakimsubiri mgombea huo kuwasili kwenye mji huo, uliopo wilayani Mbozi.
Hata hivyo, kiu ya wananchi hao kumsikiliza mgombea hiyo haikumalizwa, baada ya mkutano wake kuahirishwa saa 11 jioni kutokana na tatizo la mitambo.
Nipashe ilishuhudia maduka yakifungwa huku wengine wakisema wanaenda kumsikiliza rais wa nchi.
“Hapa mambo yote ni Lowassa...leo hakuna kazi, hakuna biashara na wala hakuna kubadilisha pesa, mambo yote ni Lowassa,” alisikika mmoja wa mashabiki hao huku akifunga duka lake.
Watu zaidi ya 20 walionekana wakiwa wamezimia uwanjani hapo kutokana na uwanja huo kufurika.
Mgombea huyo aliingia uwanjani hapo saa 10:30 jioni akipokelewa kwa shangwe wananchi hao.
HITILAFU YA MITAMBO
Akiahirisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wameamua kuahirisha mkutano huo kutokana na mitambo kugoma kufanyakazi.
“Makamanda, napenda kuwaambia kutokana na tatizo la mitambo kusumbua na vipaza sauti, naomba tumruhusu rais akapumzike ila kwa kuwa mkutano huu ni muhimu sana ni lazima ufanyike,” alisema na kusisitiza:
“Mkutano huu sasa utafanyika kesho (leo) saa 3 asubuhi hadi mitambo mingine itakapoletwa,”alisema.
WANANCHI WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tatizo hilo, baadhi ya wananchi walisema wanajua hizo ni hila za CCM.
“Haya yote yamesababishwa na serikali ya CCM mbona wenyewe wanapokuja kufanya mikutano huwa hawakati umeme, kwa nini Lowassa akifanya wanakata,” alisema John Mwamfupe na kuongeza kuwa:
“Hata wafanye nini tutampigia kura Lowassa na hatuichagui CCM...sisi tunataka mabadiliko.”
“Tunapenda kuwaambia hata wafanye nini lakini kura zote tunampa Lowassa kwani ndiyo chaguo letu.”
Naye, Joseph Samwel alisema wapo tayari kumpigia Lowassa kura licha ya kuwa watu wanamkebehi na kumtukana.
Alisema wamechoka na ufisadi unaofanywa na CCM hivyo dawa ni kufanya mabadiliko.