KIVUMBI LIGI KUU KUENDELEA JUMATANO, AZAM MGUU SAWA KUIKABILI NDANDA

KIKOSI cha Azam FC kinatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Alhamisi dhidi ya wenyeji, Ndanda FC.

Baada ya sare ya 1-1 na mabingwa watetezi, Yanga SC, Azam FC wamepania kufufua wimbi lao la ushindi keshokutwa mjini Mtwara.
Azam FC ambao walilalamikia uchezeshaji mbovu wa refa Abadallah Kambuzi wa Shinyanga Jumamosi dhidi ya Yanga SC, wataendelea kumkosa kocha wao, Muingereza Stewart John Hall siku hiyo uwanjani kwa sababu bado anatumikia adhabu yake ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katka mchezo dhdi ya Coastal Union.

Stewart atasafiri na timu na kuiandaa kama kawaida mazoezini, lakini siku ya mechi atakuwa jukwaani na mashabiki wengine kuangalia mchezo.

Azam FC inafukuzana na Yanga SC kileleni mwa Ligi Kuu, kila timu ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, wakifuatiwa na Simba SC wenye pointi 15.


Kwa ujumla, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea katikati ya wiki, Yanga SC wakiwakaribisha wanawe Toto Africans Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United na Majimaji FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, JKT Ruvu na Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Prisons na Simba SC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Coastal Union na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumatano.

Ligi Kuu itaendelea tena Alhamisi, Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mwadui FC ikimenyana na Mgambo Shooting Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati Mbeya City watakuwa wenyeji wa African Sports ya Tanga.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA