KERR AUCHIMBA MKWARA UONGOZI WA SIMBA, ADAI HAUNA UBAVU WA KUVUNJA MKATABA
Kocha wa Simba, Dylan Kerr amehoji sababu za uongozi wa klabu hiyo kumpa kipimo cha mechi mbili ili afahamu kama atabaki Msimbazi au anaondoka.
Kocha Kerr ameukosoa uamuzi huo akisema, kinachokusudiwa kufanywa uongozi wake, hakikubaliki kwa mujibu wa mkataba walioingia.
Uongozi wa Simba umemtaka kocha huyo raia wa Uingereza kuhakikisha anapata ushindi katika mechi mbili kwenye ratiba ijayo dhidi ya Coastal Union ya Tanga na Majimaji ya Songea.
Akizungumza na gazeti hili jana jijini, Kerr, alisema uamuzi wowote wa kumtimua baada ya mechi hizo mbili ni kinyume na makubaliano.
Kerr alisema mkataba alioingia na Simba ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza msimu na kushika moja ya nafasi mbili za juu.
"Najua siku moja nitaondoka Simba, lakini kwa sasa wakifanya hivi watakuwa wamekosea sana, kama kipimo ni kuangalia nafasi ya timu kwenye msimamo, hawako sahihi. Timu zilizo juu yetu tumetofautiana pointi nne, si nyingi na wakumbuke Simba imecheza mechi ngumu ugenini, wakati Azam na Yanga hawajafanya hivyo bado," alisema Kerr.
Kocha huyo alisema pia anaamini Simba itakuwa bora zaidi na kupata muda wa kujiandaa wakati mahasimu wao Yanga na Azam watakapokuwa kwenye michuano ya kimataifa.
"Simba wana nafasi ya kuongoza ligi na hata kutwaa ubingwa, tumepoteza mechi mbili lakini ni moja ya timu zenye ushindani, naamini bado nina nafasi zaidi ya kuijenga timu endapo nitaendelea kuifundisha," Kerr alisema.
Simba ilianza kufikiria kumtimua Kerr baada ya timu yao kupoteza mchezo dhidi ya Yanga na kucheza chini ya kiwango katika mechi tatu zilizopita dhidi ya Stand United, Mbeya City na Prisons.
Pamoja na kushinda dhidi ya Mbeya City na Stand United, Simba ilionyesha kiwango cha chini.
Katika kujiimarisha zaidi, klabu hiyo imesema itatumia fursa ya usajili wakati wa dirisha dogo kuleta washambuliaji.