MAKALA: NI MECHI YA KUWANIA REKODI SIMBA NA YANGA

Mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi kwenye mfululizo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

Timu hizi zilianza kupambana miaka mingi iliyopita, huku mechi zao zikivuta hisia za wapenzi wa soka nchini kabla na baada ya mechi.

Pamoja na kwamba timu hizi zimekutana mara nyingi, lakini kuna baadhi ya mechi ambazo zilikuwa na matukio ambayo hayawezi kusahaulika kirahisi.

Ni mechi ambazo zilikuwa na matukio mbalimbali ya kuhuzunisha, kuchekesha, kushangaza na nyingine kuweka rekodi ambazo hadi leo hazijafikiwa wala kuvunjwa.

Yanga ilivyoifumua Simba 5-0
Achana na ile mechi ya 2012 Simba ilipoifunga Yanga mabao 5-0. Yanga iliwahi kufanya hivyo mwaka 1968.

Ilikuwa Juni Mosi mwaka 1968,Yanga ilipoifumua Simba mabao 5-0. Magoli ya washindi yalifungwa na Maulidi Dilunga alipachika mabao mawili dakika ya 18 na 43, pia Selehe Zimbwe akifunga mawili dakika ya 54 na 89, Kitwana Manara akifunga goli moja dakika ya 86.


Simba yapata ‘uhuru’ kutoka Yanga
Iliwachukua Simba miaka mitano kuwa vibonde wa Yanga.
Hata hivyo, ilipofika 1973, Simba ilijikomboa kutoka kwenye makucha ya watani zao wa jadi baada ya kupata ushindi wa kwanza baada ya miaka hiyo kupita.

Mechi hiyo ya aina yake ilichezwa Juni 23, Simba ikishinda bao 1-0 lililofungwa kwenye dakika ya 68 na Haidari Abeid Muchacho.

Mechi ya kihistoria Nyamagana
Ni mechi ambayo haitasahaulika kirahisi na kizazi cha soka kilichokuwa hai wakati huo.
Na hata kilichozaliwa kinaikuta kwa kusimuliwa kisa cha mechi hiyo ya aina yake iliyochezwa 1974 Nyamagana mjini Mwanza.

Katika mechi hiyo ya Agosti 10, Yanga iliifunga Simba mabao 2-1 kwenye pambano kali, tata na lililokuwa na matukio ya kukumbukwa.

Simba ilielekea kuwa bingwa wakati ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Adam Sabu katika dakika ya 16. Dakika ya 87 marehemu Gibson Sembuli anaisawazishia Yanga bao.

Na kwenye dakika saba za nyongeza, Sunday Manara (baba yake mzazi Haji Manara wa Simba) akaiandikia Yanga bao la pili na Wanajangwani kutwaa ubingwa. Simba walimlalamikia sana mwamuzi, Manyoto Ndimbo, kwa madai alikuwa amezidisha muda. Mchezaji Saad Ali wa Simba akaanguka na kuzirai na kuzua uvumi kwamba eti sehemu ile aliyoangukia hapaoti majani huku wengine wakidai kuna kichuguu. Shabiki mmoja wa Simba alijitumbukiza kwenye pipa la mafuta na kufariki baada ya timu yake kupoteza mechi hiyo.

Simba yaibebesha Yanga 6-0
Hii ndiyo mechi ambayo inawaumiza vichwa Wanayanga wote hadi hii leo.

Hawajui ni lini wanaweza kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 6-0 ambayo walifungwa 1977.
Pambano hili la aina yake lilichezwa Julai 19, na kuweka rekodi ambayo hadi leo hakuna mchezaji yoyote aliyeivunja.

Alikuwa ni mshambuliaji hatari wakati huo, Abdallah ‘King’ Kibadeni (sasa ni kocha) aliyefunga ‘hat trick’ kwenye mechi hiyo.

Alifunga katika dakika ya 10, 42 na 89 na kuweka rekodi ambayo haijavunjwa kwa mchezaji yoyote kati ya timu hizo mbili kwa miaka 38 sasa.

Magoli mengine ya Simba yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ akifunga mawili dakika ya 60 na 73, huku beki wa Yanga, Selemani Sanga, akijifunga katika dakika ya 20.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA