MAKALA: Halifa Maliyaga: Msanii anayekuja juu bongo muvi
Na Prince Hoza
ONGEZEKO la vijana katika tasnia ya sanaa hasa filamu limezidi kukua kwa kasi, hii inadhihirisha kuwa vijana wengi hawana ajira na sasa filamu zinaweza kuwaokoa.
Halifa Yuda Maliyaga ( Pichani) ndiyo jina lake halisi, naye ameamua kujikita kwenye tasnia hiyo lakini yeye anadai sanaa hiyo ipo ndani ya damu ya ukoo wao kwani kaka yake Hemed Halifa Maliyaga maarufu 'Mkwere' anatesa kwenye kundi la Mizengwe.
Maliyaga aliingia rasmi kwenye sanaa baada ya kumaliza shule ya msingi mwaka 2011 katika shule ya Mdaula Chalinze Pwani, kundi lake la kwanza kushiriki nalo linaitwa Zinduko Arts ambapo alidumu nalo hadi mwaka 2014.
Maliyaga alijiunga na kundi la Nuru njema Arts Group mwaka 2014 ambapo anatamba nalo hadi sasa.
NINI KILIMSUKUMA KUINGIA KWENYE SANAA HIYO
Moja ya sababu zilizomfanya aipende tasnia hiyo ni ushawishi mkubwa baada ya kumuona ndugu yake Hemed Halifa maarudu 'Mkwere' akitamba katika fani hiyo/
Amesema katika kipindi hiki toka awepo kwenye sanaa ya uigizaji ameshashiriki kurekodi filamu nne ambazo alizitaja ni 'Tandu', 'Mti wa ajabu', 'Bonge la utata' na 'Mfalme puto' ambao unatarajia kutoka baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu Ramadhani.
CHANGAMOTO
Maliyaga amesema changamoto ni nyingi kwa wasanii chipukizi kama wao lakini kikubwa ni nidhamu na uvumilivu, na amemtaja msanii Gabo kwamba ndiye anayemvutia.
Amemaliza kwa kusema, lengo lake ni kuwa mmoja wa wasanii wakubwa katika nchi hii kama ilivyo kwa kaka yake Mkwere anayetesa ITV na kundi lake la Mizengwe.