MGAMBO SHOOTING YAAPA KUSIMAMISHA SIMBA, MKWAKWANI LEO
Simba itakuwa na kibarua kigumu mbele ya 'maafande' hao kutoka kitongoji cha Kabuku wilayani Handeni, timu hizo zitakapochuana katika mechi ya kiporo ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa.
Mechi hiyo Na. 62 ya raundi ya 9 ya VPL, ilipaswa kuchezwa Januari 4, lakini ikapigwa kalenda kutokana na kufinyangwa finyangwa kwa ratiba ya ligi hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sanjari na ushiriki wa Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwanzoni mwa mwaka.
Katika mahojiano na mtandao huu jijini hapa jana mchana, Shime alisema kikosi chake kiko tayari kukabiliana na Simba na kulinda rekodi yao ya kutopoteza mechi hata moja dhidi ya timu kongwe nchini Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani tangu kipande ligi kuu misimu miwili iliyopita.
Alisema Simba wana kikosi kizuri kilichoshinda mechi tatu mfululizo tangu kifungwe 1-0 dhidi ya Stand United usukumani mjini Shinyanga, lakini haikihofii kwa sababu timu yake nayo ina rekodi nzuri ikiwa imepoteza mechi moja tu katika mechi nne zilizopita.
"Tuna wachezaji 22 ambao wote wako tayari kwa mechi ya kesho (leo), ni kuchagua tu acheze nani. Tumefuatilia mechi za Simba, wameimarika ingawa mabao yao katika mechi mbili zilizopita yalifungwa pasipo kutarajia.
"Tuna rekodi nzuri hapa Tanga dhidi ya Simba, lakini kesho hatutazizingatia. Itakuwa vita ya dakika 90 ya Mgambo dhidi ya Simba bila kujali kipindi cha nyuma kulitokea mambo yepi," alisema zaidi Shime.
Alipotafutwa na NIPASHE jijini hapa jana mchana kuzungumzia mechi ya leo, kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, alisema: "Mimi siruhusiwi kuzungumzia masuala ya timu ya Simba kwa sasa, mtafute kocha mkuu."
Kikosi cha Mgambo ambacho leo kinajaribu kuisimamisha Simba kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga
Goran Kopunovic, kocha mkuu wa Simba, alisema kuwa mechi ya leo itakuwa ngumu kwa kikosi chake kutokana na ubovu wa Uwanja wa Mkwakwani, lakini watapambana ili washinde.
Alisema tangu atue Msimbazi na kusaini mkataba wa miezi 6, amebaini kuwa timu 'ndogo' zimekuwa zikikamia timu yake hasa inapocheza nje ya Dar es Salaam.
Simba wanaotambia makali ya mshambuliaji wao Mganda Emmanuel Okwi wanasaka ushindi leo ili kulipa kisasi cha kufungwa na Mgambo jijini wakati timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nayo ikisaka kisasi cha kufungwa na Simba mabao 6-0 jijini Dar es Salaam msimu uliopita.
Wanamsimbazi leo pia watakuwa na mshambuliaji wao wenye 'hat-trick' pekee msimu huu, Ibrahim Ajibu, anayerejea uwanjani baada ya kukosa mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na kuwa na kadi nne za njano.
Mgambo huwa haipotezi mechi kirahisi mzunguko wa pili kwenye uwanja wa nyumbani. Msimu uliopita ilichukua pointi zote 6 dhidi ya Simba (1-0) na Yanga (2-1)kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Msimu wa 2012/13 Mgambo ilitoka suluhu dhidi ya Simba kabla ya kuinyuka timu hiyo bao 1-0 msimu uliopita.