MAKALA: SIMBA HAIWEZI KUTWAA UBINGWA WA BARA MSIMU HUU


Ni dhahiri kuwa ikiwa na pointi 32 kibindoni, Simba itamaliza msimu wa tatu bila taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kimahesabu, Simba ambayo tayari imecheza mechi 20 ikilinganishwa na 19 za Yanga yenye pointi 40 na 18 ya Azam yenye pointi 36 haiwezi kutwaa ubingwa, isipokuwa kama Yanga au Azam zitapoteza mechi nne kati ya zile walizobaki nazo.

Endapo Azam yenye mechi nane ikipoteza mechi nne itamaliza ligi ikiwa na pointi 48, huku Yanga yenye mechi saba ikipoteza nne, itakuwa na pointi 49 na Simba ikishinda mechi zake zote sita ilizobakiwa nazo, itakuwa na pointi 50, hivyo itaibuka bingwa.


Hata hivyo, Simba ilianza vibaya msimu kwa sare saba, kabla ya kuzinduka kwa kuichakaza Prisons, mabao 5-0 na Yanga 1-0, lakini ikapotea tena kwa kufungwa na Mgambo bao 1-0.

Hadi sasa, Yanga inahitaji sare dhidi ya Azam na kushinda michezo mingine minne ili ijitangazie ubingwa wake wa 25 katika msimu huu utakaomalizika Mei 9.

Yanga yenye pointi 40 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36 inaonekana kutokamatika kirahisi kutokana na moto waliouonyesha kwenye ligi.

Bingwa mtetezi, Azam ina michezo mingi mkononi kuliko wapinzani wake wote, imebakiwa na michezo minane, wakati Yanga imebakiwa na michezo saba na Simba ikibakiwa nayo sita.

Pamoja na Azam kuwa na michezo mingi, bado Yanga inaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa kama itapiga vizuri hesabu zake kuanzia sasa.

Kama Yanga itashinda michezo yake saba iliyobaki, ikiwamo dhidi ya Azam, Mei 6, itafikisha pointi 61, itakuwa bingwa kwani Azam haitaweza kuzifikia pointi hizo, hata kama ikishinda michezo saba, itamaliza ligi ikiwa na pointi 57.

Kocha wa Simba Mcroatia Goran Kopunovic anapaswa kuandaa kikosi cha msimu ujao kwani tayari ubingwa unanukia kwa Yanga au Azam

Pia, Yanga ikishinda mechi sita, ikiwamo ile ya Azam, itakuwa bingwa ikiwa bado na mchezo moja mkononi, itafikisha pointi 58, ambazo haziwezi kufikiwa na Azam, hata kama itashinda michezo yote saba kwani itafikisha pointi 57.

Kitakwimu, Yanga ina nafasi zaidi ya ubingwa kwani hata kama ikishinda michezo sita na kutoa sare na Azam, itakuwa bingwa kwa pointi 59, ambazo haziwezi kufikiwa na Azam, hata kama ikishinda michezo saba na sare moja, itamaliza ligi ikiwa na pointi 58.

Ili Azam itetee ubingwa wake, inatakiwa kushinda michezo yake yote minane iliyobaki, ikiwamo kuifunga Yanga, Mei 6 zitakapokutana na kufikisha pointi 60, ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wake hao, hata kama Yanga itashinda michezo sita itafikisha pointi 58.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA