PLUIJM APONDA MASTRAIKA WACHOYO YANGA

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amewajia juu washambuliaji wa timu hiyo kutokana na kukosa magoli mengi na amewataka kuacha uchoyo baina yao kwa manufaa ya timu.

Licha ya kushinda kwa idadi kubwa ya mabao (4-0) katika mechi zao mbili za kwanza za Kombe la Mapinduzi, wachezaji wa Yanga walikuwa wakikosa magoli mengi ambayo yangeweza kuwafanya kupata ushindi mnono zaidi.

Yanga ilitolewa katika robo fainali ya mashindano hayo maalum ya kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa goli 1-0 la dakika za lalasalama la JKU ya Zanzibar huku miamba hao wa soka wa Tanzania Bara wakiwa tayari wamekosa magoli mengi kupitia kwa washambuliaji wao Amisi Tambwe na Kpah Sherman.


Akizungumza jana katika makao makuu ya klabu hiyo Jangwani jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Bagamoyo kuweka kambi ya kujiandaa na mechi yao ua Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Ruvu Shooting, kocha huyo Mholanzi alisema amebaini kuna tatizo la ushirikiano katika umaliziaji na aliwataka washambuliaji kushirikiana zaidi ya sasa.

Alisema amewaelezea wachezaji wake kwamba ni lazima washirikiane kwa sababu mafanikio ama kushindwa kunakuwa ni kwa timu nzima na si mchezaji mmoja mmoja, hivyo waweke mbele kusaka mafanikio ya pamoja.

Pluijm alisema walipoteza nafasi nyingi za kufunga katika mechi zao za Kombe la Mapinduzi na kwamba hatapenda kuona mapungufu hayo yanajirudia katika Ligi Kuu ya Bara.

"Tunajitahidi kurekebisha makosa madogo yaliyojitokeza katika Kombe la Mapinduzi ili iwe tofauti tutakaporejea kwenye Ligi  Kuu," alisema Pluijm.

Akizungumzia maandalizi ya mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, alisema timu hiyo ya mkoani Pwani siyo ya kubeza licha ya kwamba msimu uliopita waliifunga 7-0 katika mechi ya ligi kuu.

"Hakuna mechi nyepesi msimu huu, utaona timu kubwa inafungwa dhidi ya timu ndogo, kinachotakiwa ni maandalizi na kupanga kikosi imara," alisema Mholanzi huyo aliyerejeshwa kuchukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo aliyetimuliwa baada ya mechi saba tu za mzunguko wa kwanza.

Alisema kikosi chake kimebadilika tangu aanze kukifundisha na kwamba anachofanya ni kuendelea kufanyia kazi mapungufu machache ili kiwe tishio kwenye ligi.

Alisema atahakikisha timu yake haipotezi mechi kuanzia mchezo wao ujao Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting na mechi inayofuata dhidi ya Coastal Union Jumatano ijayo ugenini Tanga.

Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 14, mbili nyuma ya vinara Mtibwa Sugar.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA