KOPUNOVIC AAHIDI KUTINGA FAINALI LEO NA POLISI ZANZIBAR

Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic amesema kikosi chake kimeimarika na kinampa matumaini ya kushinda mechi yao ya leo ya nusu-fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Polisi na kutinga fainali ya michuano hiyo.

Mechi hiyo itatanguliwa na mechi ya nusu-fainali ya kwanza ya Mtibwa Sugar dhidi ya wababe wa Yanga, timu ya JKU, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa saa 10:00 jioni na saa 2:15 usiku.

Goran alisema visiwani hapa jana kuwa: “Kikosi chetu kinazidi kuimarika, jana (juzi) tulianza mazoezi maalum kwa ajili ya mechi ya nusu-fainali na ninaona tuko katika hali nzuri."

"Kuna vijana wazuri nimewakuta kikosini, ninaamini tutafanya vizuri na kusonga mbele,:" alisema zaidi Mserbia huyo.

Simba ilifanikiwa kutinga nusu-fainali ikiiadhibu kwa kipigo hicho kikali timu ya Daraja la Pili visiwani hapa Taifa ya Jang'ombe katika mechi yao ya robo-fainali Jumatano, shukrani kwa mabao ya kiungo mshambuliaji Ibrahim Hajibu aliyepiga 'hat-trick' dakika za 46, 62 na 75 kabla ya kiungo mshambuliaji Shaba Kisiga kufunga la nne dakika 10 kabla ya nusu sasa ya tatu ya mchezo.


Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti hili visiwani hapa jana mchana, Kocha Mkuu wa Polisi, Hamis Sufian alisema: "Nimekuwa nikitumia muda mwingi kuangalia mechi za Kombe la Mapinduzi. Nilifanikiwa kuisoma vizuri KCCA. Wembe uliotumika kuinyoa, ndiyo ule ule utakaotumika kuinyoa Simba maana nao pia nimewasoma."

Polisi imetinga nusu-fainali baada ya kuwavua ubingwa kwa matuta KCCA ya Uganda katika mechi kali ya robo-fainali iliyomalizika kwa suluhu katika dakika 90 za kawaida.

MTIBWA vs JKU NI VITA

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema anazitambua vyema mbinu za Kocha Mkuu wa JKU, Malale Hamsini ambaye leo timu zao zinapambana katika mechi ya kwanza ya nusu-fainali.

"JKU ni timu nzuri na ngumu, ina mfungaji mzuri (Amour Omary) Janja ambaye nimemuona hapa anafunga mabao mazuri. Goli lake la jana ninafikiri ni bao bora la mashindano haya mwaka huu.

"Kocha Mkuu wa JKU ni 'classmate' (mwanafunzi mwenzake) wangu katika ukicha. Ninazifahamu mbinu zake na yeye anazijua za kwangu. Mashabiki waje waone kitakachotokea maana na sisi tuna kikosi kizuri msimu huu," alisema Mexime katika mahojiano maalum na gazeti hili visiwani hapa jana mchana.

Baada ya kuing'oa Yanga juzi, Malale alisema atajipanga vizuri kuhakikisha anakuwa kocha wa kwanza kuifunga Mtibwa katika mechi za mashindano msimu huu.

Mtibwa na JKU zilikutana katika mechi ya mwisho ya Kundi B iliyomalizika kwa sare ya bao moja, mabao yakifungwa na Mussa Hassan 'Mgosi'dakika ya 20 na baadaye alikosa penalti kabla ya 'mbaya wa Yanga', Janja kuisawazishia timu yake dakika ya 72.

Safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar inayoongozwa na mchezaji bora wa mechi iliyopita ya robo-fainali dhidi ya Azam FC, Salim Mbonde, inapaswa kumchunga kwa uangalifu mkubwa Janja kwani mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita na kinara wa mabao kwa sasa katika ligi hiyo(mabao nane) ana miguu inayolijua goli lilipo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA