MAKALA>>>NANI APEWE MECHI MBILI, PHIRI AU ALIYEMSAJILI KWIZERA!

Na Frank Sanga

BAADHI ya wachezaji wa Simba wanamaliza mikataba Desemba mwaka huu na wengine wamebakiza miezi sita hivyo wanaweza kufanya mazungumzo na klabu yoyote.

Tunaambiwa kuwa hata Jones Mkude, ambaye ni tegemeo lao kuu yupo ndani ya miezi sita kumaliza mkataba wake katika mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Najua mashabiki wa Simba wasingependa kusikia habari hizi, wala wasingependa kusoma habari ya aina hii, lakini huo ndio ukweli ambao ni lazima ukubaliwe.

Ni kama uongozi wa Simba umechanganyikiwa, haujui ufanye nini na ndio maana tunashuhudia mambo mengi yakitokea katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Uongozi hauelewi ufanye nini? Kuna uwanja ambao tuliambiwa uko Bunju, lakini ilikuwa ni mbwembwe tu hakuna unaloweza kujivunia mpaka sasa katika mradi huo.


Katika kupaniki huko, uongozi umejikuta ukimpa mechi mbili kocha wao Patrick Phiri ashinde vinginevyo atafungashiwa virago kurudi kwao Zambia.
Wakati kocha akipewa mechi mbili, uongozi huohuo unawafungia wachezaji watatu mahiri; Amri Kiemba, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo.

Nimebaki najiuliza itakuwaje Phiri akashinda mechi mbili wakati uongozi umewaondoa wachezaji watatu wa kikosi cha kwanza? Wanataka awatumie wachezaji gani kushinda.

Ni kama kumwambia jenerali wa jeshi ashinde vita halafu wakati huohuo unawafukuza makamanda wake.

Lakini tujiulize, ni nani anastahili kutoa adhabu kwa wachezaji? Ni uongozi wa klabu au ni kocha? Ni maswali ambayo jibu lake ni rahisi tu; kwa mfumo unaoeleweka kocha ndiye bosi wa timu.

Huwezi kusajili wachezaji wa kigeni wanaokaa benchi halafu ukamlaumu kocha eti kwa kutofanya vizuri wakati hakuhusika hata kidogo kufanya usajili wa wachezaji.

Kama kiongozi alimsajili Pierre Kwizera anayekaa benchi, unamlaumu vipi Phiri kwa matokeo mabaya ya uwanjani? Kwanini asichukuliwe hatua aliyefanya usajili mbovu?

Tatizo kubwa Simba hawajui thamani na ubora wa Phiri katika soka la kimataifa. Phiri amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia. Si kitu kidogo kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia tena kwa vipindi viwili tofauti.

Zambia ipo juu kisoka kuliko Tanzania, ina historia kubwa katika soka, ina vipaji vingi, lakini bado walimuamini Phiri na kumfanya awe kocha wao wa timu ya taifa mara mbili.

Kuchanganyikiwa kwa uongozi ndio kumewafanya wamuone Phiri hafai na hata kutoa kauli ya kitoto kuwa wanampa mechi mbili kocha huyo wa zamani wa Nkana Red Devil.

Nadhani Simba imefukuza sana makocha, imesimamisha sana wachezaji tangu enzi na enzi, sasa ni wakati wa kuanza kuwatimua viongozi wasiojua wajibu wao na kwa kuanza ni vyema wangetimuliwa wale waliofanya usajili msimu huu.

Timu itacheza vipi mpira kama wachezaji wanatishwa, hawana raha, wanasingiziwa kuhujumu mechi na hawana uhakika wa siku inayofuata?

Mbona Azam na Yanga zimepoteza mechi mbili na hatujasikia malalamiko yoyote. Unaweza kuamini kama Azam inaweza kupoteza mchezo kwa JKT Ruvu au Ndanda United?

Hapa kuna kitu kimoja tu, uongozi Simba uache kuchanganyikiwa, uonyeshe ukomavu na badala ya kuwa na visingizio lukuki wajiangalie wao kwanza na wamuache Phiri afanye analoliweza ikiwa ni pamoja na kupanga kikosi anachokitaka. Kama ni kufukuzana waanze kwa aliyemsajili Kwizera.


Makala hii imeandikwa na Frank Sanga wa gazeti la Mwanaspoti


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA