JONAS MKUDE MBIONI KUTUA YANGA, AZAM NAYO YAMTAKA NDEMLA

SIMBA huenda wakapata pigo kubwa kama hawatafanya jitihada za kukaa chini na wachezaji wao muhimu ambao mikataba yao iko ukingoni.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Jonas Mkude na Said Ndemla ambao kwa sasa wanaruhusiwa kufanya mazungumzo ya awali na klabu yoyote.

Gazeti hili linajua kuwa Simba walianza mikakati jana Jumapili ya kuweka mambo sawa lakini wapinzani wao Yanga na Azam wameshashtukia dili na ndio wanafanya mikakati ya chinichini kuwanasa wachezaji hao muhimu kwa Simba.

Habari za uhakika kutoka Yanga ambazo gazeti hili inazo ni kwamba wameelekeza nguvu zao kwa Mkude huku wakisisitiza kwamba ndiye mchezaji pekee wa Simba kwa sasa mwenye hadhi ya kuichezesha na kusukuma mashambulizi kwenye mzunguko wa pili wa ligi na Kombe la Shirikisho ikielezwa kwamba hata mfumo wa Marcio Maximo unambeba.


Habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba zinadai kwamba tofauti zilizopo kati ya wanachama wa kundi la Friends of Simba huenda zikaigharimu timu hiyo kwani baadhi yao wamekuwa wakivujisha siri za uongozi kwa wapinzani wao Yanga wanapokuwa vijiweni.

Mbaya zaidi imedaiwa kwamba baadhi yao ndio wanaowaondoa Ndemla na Mkude Simba kwani wameanza kutafuta mpaka timu na kuwasaidia wachezaji hao ushauri ili kuwakomoa viongozi wenzao kwa kile kinachodaiwa kwamba wamewaweka pembeni na hawataki kuyafanyia kazi mawazo yao kwenye mambo mbalimbali.

Azam yenyewe imedaiwa kwamba imemtengea Ndemla Sh40 milioni kwavile mkataba wake una miezi sita kama ilivyo kwa Mkude. Kwa mujibu wa kanuni za usajili mchezaji anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine anapobakiza miezi sita, hivyo ni rahisi sasa kuanza mazungumzo na klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara endapo wapo tayari kuondoka Simba.

Habari kutoka ndani ya Yanga ilisema kuwa wanasubiri ripoti ya kocha wao Mbrazil Marcio Maximo ambayo itatoka baada ya kumaliza mechi mbili zijazo dhidi ya Mgambo na Azam. Lakini Azam na Ndemla wameshaanza mazungumzo.

Dirisha dogo la usajili linatarajia kufunguliwa rasmi Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka huu, hivyo kila timu kwa sasa inatafuta jinsi ya kupata wachezaji wazuri wa kuimarisha vikosi vyao.

Yanga ina tatizo la kiungo mkabaji na hivyo kulazimika kumtumia Mbuyu Twite ambaye anamudu zaidi kucheza nafasi ya beki wakati Azam kama watamsajili Ndemla basi atakabiliana na upinzani kutoka kwa Salum Aboubakar ‘Sure Boy’.

“Tunasubiri ripoti ya kocha Maximo, lakini tumejaribu kuangalia ni mchezaji gani anaweza kutufaa, kwa pale Simba ni Mkude pekee hakuna mwingine, safu yetu ya kiungo inatakiwa kuimarishwa ila hatuwezi kuamua wenyewe mpaka kocha ashirikishwe,” alisema kiongozi huyo wa Yanga.

Wakati Mkude na Ndemla wakibakiza muda mfupi kuichezea Simba imeelezwa kuwa wachezaji wengi waliosajiliwa kutoka U-20 akiwemo Ramadhan Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo ni miongoni mwa wachezaji wanaomaliza mikataba yao.

Yanga na Azam zikiwa kwenye mpango wa kuibomoa zaidi Simba ambayo mwenendo wake kwenye ligi ni wa kusuasua, Simba wao wamesema watahakikisha wanafanya jitihada za kuwafunga wachezaji hao kwa kuwapa mikataba mipya ingawa imedaiwa kuwa mchezaji kama Chanongo wanaweza kuachana naye.

“Ni kweli wachezaji hao Ndemla na Mkude wapo ndani ya mikataba ya miezi sita lakini kuna wengine ambao walitoka U-20 (sio kipindi hiki cha Rais Evans Aveava) nao wanamaliza mikataba yao na hapo hapo baadhi yao hawajamaliziwa fedha yao ya usajili akiwemo huyo Ndemla,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA