YANGA YAANZA KAZI,COUTINHO HABARI NYINGINE



Yanga ilipata ushindi wake wa kwanza wa ligi msimu huu baada ya kuifunga timu iliyobakiwa na wachezaji 10 uwanjani ya Tanzania Prisons kwa magoli 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Kiungo Mbrazil Andrey Coutinho aliiandikia Yanga goli la kwanza katika dakika ya 34 kwa shuti kali la mguu wa kushoto lililompita ubavuni kipa Mohamed Omary. Mbrazil huyo aliyekosa mechi ya ufunguzi waliyopigwa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita, aliachia kombora hilo la umbali wa takriban mita 25 wakati akipiga 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni.

Dakika tano baada ya goli hilo, Prisons walilazimika kucheza pungufu baada ya Jacob Mwakalabo kutolewa kwa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kumkwatua winga Mrisho Ngasa nje kidogo mwa boksi la maafande hao. Mchezaji huyo pia alionywa pia kwa kadi ya njano dakika ya 24 baada ya kumkwatua kiungo Haruna Niyonzima katikati ya uwanja.


Hadi mapumziko, Yanga ilikuwa mbele kwa goli hilo. Kipindi cha pili, licha ya kubaki 10 uwanjani, Prisons ilianika udhaifu wa wenyeji wao wakati iliposawazisha goli hilo kupitia kwa mtokea benchini Ibrahim Kahaka aliyeunganisha kwa kichwa krosi murua ya Jeremia Juma katika dakika ya 67.

Hata hivyo, goli hilo lilidumu kwa dakika tano tu kwani dakika ya 72, winga Simon Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya Coutinho aliwafungia wenyeji goli la pili akimalizia kwa kichwa krosi safi ya mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita, Ngasa.

Baada ya mechi hiyo, kocha wa Prisons, David Mwamaja alisema: "Hakututendewa haki katika baadhi ya maamuzi. Inabidi chama cha marefa waangalie kwa umakini uchezeshaji wa marefa ili unapoondoka uwanjani uwe umeridhika umefungwa kihalali."

Kocha ya Yanga, Mbrazil Marcio Maximo alisema timu yake ilistahili kushinda mechi hiyo baada ya kuanza msimu vibaya ugenini Morogoro wiki iliyopita.
"Ninaipongeza Tanzania Prisons kwa mchezo mzuri, hakika wana timu nzuri. Tumeshinda kwa sababu tulistahili kushinda. Tulitengeneza nafasi nyingi za magoli lakini wachezaji wetu wametumia chache. Tutaendelea kutengeneza kikosi imara," alisema.

Baada ya mechi, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alijikuta katika wakati mgumu baada ya kupigwa na chupa ya maji usoni kutoka kwa shabiki.

Tukio lilianza pale Cannavaro alipoonekana kumnyooshea mkono mmoja wa mashabiki waliokuwa kwenye jukwaa la Simba karibu na lango kuu la kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mechi na shabiki huyo (jina halikufahamika) kujibu kwa kumpiga kwa chupa ya maji nahodha huyo wa Yanga na Taifa Stars.

Mtandao huu ulishuhudia baada ya tukio hilo shabiki huyo akisindikizwa na askari polisi watatu na baunsa mmoja hadi kwenye gari la polisi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.

Akizungumzia tukio hilo baada ya kutafutwa na gazeti hili, Cannavaro alisema: "(Shabiki yule) Aliniuliza kwa nini nimeokoa goli dakika za mwisho, kisha akanipiga chupa ya maji. Ninashukuru Mungu sijaumia."

Takwimu za baada ya mechi zilionyesha kwamba yanga walitawala mchezo kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Prisons wakati Yanga ilipiga mashuti sita yaliyolenga lango dhidi ya manne yaliyolenga lango. Mashuti ya Yanga yaliyoenda nje ya lango yalikuwa 4-4. Yanga walipata kona 9 dhidi ya 4 za Prisons huku Yanga walicheza faulo 12 wakati Prisons walicheza faulo 15. Yanga waliotea mara 6 huku Jaja akinaswa mara nne kati ya hizo. 

Prisons hawajawahi kuifunga Yanga kwenye Uwanja wa Taifa tangu wapande ligi kuu. Msimu wa 2012/13 walifungwa 3-1 na msimu uliopita walifungwa 5-0 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558.

Waliwahi kuifunga Yanga 4-2 kwenye Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine na kuikosesha ubingwa 2004/5 huku wakitoka sare ya bao 1-1 msimu uliopita kwenye uwanja wao wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 21,000.

Katika mechi nyingine iliyochezwa jana, Kagera Sugar ilishinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam. Magoli ya Kagera yalifungwa na Salum Kanoni kwa njia ya penalti katika dakika ya 9 na Rashid Mandawa dk 79.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Yanga: Deogratius Munishi ' Dida', Juma Abdul, Edward Charles, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani/ Rajab Zahir (dk 78), Mbuyu Twite, Said Dilunga/ Hamis Thabiti (dk 56), Haruna Niyonzima, Gilson Santos Santana 'Jaja', Mrisho Ngasa na Andrey Coutinho/ Simon Msuva (dk 58).

Prisons: Mohamed Omary, Salum Kimenya, Laurian Mpapile, Nurdin Chona, Lugano Mwangama, Jumanne Hifadhi, Meshack Olesti/ Julius Kwangwa (dk 35), Fred Dunga/ Ibrahim Kahaka (dk 53), Jacob Mwakalabo, Amri Omary/ Boniface Hau (dk 53) na Jeremia Juma.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA